Waziri Mwambe awapa neno maafisa Biashara nchini, Afungua semina ya mafunzo Jijini Dodoma


 


WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji Geoffrey Mwambe,amewataka Maafisa biashara nchini kuacha tabia ya kufunga maduka ya wafanyabiashara wanaodaiawa kwani kufanya hivyo ni kosa sawa na uhujumu uchumi.

Hayo ameyasema leo June 29,2021 jijini Dodoma wakati akifungua semina ya mafunzo kwa Maafisa biashara wa mikoa kilichoandaliwa na kituo cha taifa cha uwekezaji (TIC).

Waziri Mwambe amesema kuwa kitendo cha Maafisa biashara kufunga maduka ya wafanyabiashara kutokana na kudaiwa mapato au kuisha kwa leseni amesema siyo jambo la busara.


“Unakuta mtu anadaiwa fedha kiasi kidogo tuu labda leseni yake imeisha siku chache zilizopita lakini afisa biashara anafunga duka na kufuri jambo hili ni sawa na ilivyo katika kosa la uhujumu uchumi”amesema  Mwambe.

Mwambe ametumia semina hiyo kuwaasa Maafisa Biashara hao kutumia taaluma na weledi wao katika kutafuta wawekezaji kwenye Mikoa yao lakini pia kuwa daraja la wawekezaji kuwekeza.

” Nyinyi mna nafasi kubwa ya kuchochea maendeleo kwenye Nchi yetu kama kila mmoja kwa nafasi yake ataamua kwa dhati kutumia weledi na taaluma yake kutafuta wawekezaji.

Nchi yetu ina utajiri sana hakuna sehemu yoyote kwenye Nchi yetu ambayo haina soko la kibiashara, kama siyo Madini basi ni Utalii, Kilimo au hata Viwanda, nyanyueni uwekezaji kwenye Mikoa yenu,” Amesema Waziri Mwambe.

Amesema pia Wizara yake iko katika mpango wa kuwezesha Maafisa Biashara kuwa wasimamizi wa zile asilimia 10 wanazogaiwa makundi maalum ya Wanawake, Vijana na Wenye Ulemavu.

” Nafikiri kuna haja ya zile asilimia 10 za makundi maalum ziwe zinasimamiwa na Maafisa Biashara maana haiwezekani Maafisa Maendeleo ya Jamii ndio wasimamie watu biashara wakati siyo taaluma zao,” Amesema Waziri Mwambe.


Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa kituo cha uwekezaji Tanzania Dk. Maduhu Kazi, amesema kuwa lengo la semina ya mafunzo hayo ya siku mbili ni kujifunza na kubadilishana uzoefu katika masuala ya uwekezaji.


Naye  Afisa Biashara wa Mkoa wa Mbeya Stanley Kibakaya akitoa neno la shukrani kwa niaba ya Maafisa Biashara wenzake amemuahidi Waziri Mwambe kwamba wataenda kufanya kazi kwa bidii huku wakiwa sehemu ya watekelezaji wa mpango wa Tatu wa Taifa wa Maendeleo kwa bidii na weledi.

” Tunakushukuru Mhe Waziri kwa nafasi hii uliyotupatia, semina za mafunzo kama hizi zimekua zina manufaa makubwa na tunaomba ziendelee kuwepo mara kwa mara,” Amesema Kibakaya.

Comments