Naibu Waziri Ummy amtaka OCD Pangani kuwakamata wanaowaibia baiskeli watu wenye ulemavu


NAIBU Waziri,Ofisi ya Waziri Mkuu (Watu Wenye ulemavu) Ummy Nderiamanga amemtaka Mkuu wa Polisi wilaya ya Pangani (OCD) kuhakikisha watu wanaowaibia baiskeli watu wenye ulemavu wanakamatwa na kuchukulia hatua kali za kisheria.

Ummy aliyasema hayo wilayani Pangani wakati wa ziara yake ya siku moja iliyoambatana na kutembelea maeneo mbalimbali ya watu wenye ulemavu ikiwemo kikundi cha Huruma Disiability na kuzungumza nao kwenye ukumbi wa zamani wa Halmashauri hiyo.

Alisema haiwezekani watu wenye ulemavu wakabuni miradi yao ya kukodisha baiskeli ili waweze kujikwamua kiuchumi huku watu wengine wakikwamisha juhudi hizo hivyo ni lazima washughulikiwe kwa mujib wa sheria zilizopo

“Katika Taarifa ya Mkuu wa wilaya nimesikia hapa kwamba kuna changamoto ya wenye ulemavu wakikopesha baiskeli watu wanaingia mitini Mkuu wa Polisi wilaya ya Pangani (OCD) naomba watu hao washughulikiwe”Alisema Naibu Waziri Ummy.

Alisema suala hilo analichukulia kwa namna mbili la kwanza ni uonevu na udhalilishaji wa watu wenye ulemavu kwamba hawawezi kukimbia lakini pia wizi kama wizi mwengine hivyo wachukulie hatua kali ili lisiwezi kujitokeza tena kwa sababu leo ni baiskeli kesho wataenda kwa wale wenye migahawa na kuweza kuchukuwa hela zao.

Hata hivyo aliendelea kuwatia moyo na kuwahamasisha watu wenye ulemavu hususani wanafunzi wa kike maeneo ya pwani mambo ya shule yapo nyuma watoto wa kike wenye ulemavu wahakikishe wanasoma kwa bidii lakini pia watumieni mifano hata kama hii ya kwetu wanaweza kufika mbali.

Awali akizungumza wakati akitoa taarifa ya wilaya hiyo kwa Naibu Waziri huyo,Mkuu wa wilaya ya Pangani Ghaibu Lingo alisema changamoto zinazowakabili watu wenye ulemavu ni baadhi yua wateja kutokuwa waaminifu wakikodishwa baiskeli kutokurudisha ikiwemo katika kikundi cha Huruma Disiability kupata hasara ya kuibiwa baiskeli moja na kesi ipo Polisi

Comments