Na Amiri Kilagalila,Njombe.
Kesi za utelekezaji,ulawiti,ubakaji na unyanyasaji wa kingono umetajwa kuongeza kiwango cha ukatili katika halmashauri ya wilaya ya Njombe hadi kufikisha matukio ya ukatili wa kijinsia 161 katika kipindi cha miaka miwili ya 2019/2020 na 2020/2021.
Taarifa hiyo imebainishwa na afisa ustawi wa jamii halmashauri ya wilaya ya Njombe Avelino Chaula kabla ya mkutano wa baraza la madiwani wa halmashauri hiyo uliofanyika katika ukumbi wa shule ya sekondari Mtwango na kulazimika kutoa elimu kwa madiwani na wajumbe wa baraza hilo juu ya ulinzi na usalama wa mtoto kwa madiwani na maofisa watendaji wa kata na kwamba katika matukio hayo yote lakini matukio ya utelekezaji yameripotiwa mengi zaidi kuliko mengine.
“Kwa miaka miwili tuna matukio 161 lakini matukio yanayoongoza kwa wingi ni ya utelekezaji na ukiangalia matukio ya utelekezaji kwa mwaka wa kwanza tuna matukio 42,na mwaka wa fedha 2020,2021 tuna matukio 57 na haya ni kwa yale yaliyotufikia ofisini sasa tujiulize ni mangapi hayajafika?tuombe wazazi wawajibike kulea watoto”alisema Chaula.
Kutokana na hali hiyo baadhi ya madiwani wa kata mbalimbali akiwemo Neema Mbanga, Isaya Myamba na Roida Wandelage wametaka kuwekwa kwa mikakati maalumu ya kushughulikia changamoto za ukatili ikiwemo tatizo la kesi nyingi za ujauzito wa watoto kutomalizika.
“Watoto wengi wanapita mimba lakini ukianza kufuatilia unaona tu imeishia hewani kwa hiyo ninaomba halmashauri tuweze kuwa makini na kuyafuatilia haya kwa nguvu zote”alisema Neema Mbanga
“Nadhani kuna sababu ya msingi ya kujipanga upya namna ya kudhibiti na kushughulikia kesi hizi kuhakikisha zinaisha”Alisema Isaya Myamba
Naye Roida Wandelage alisema “Mtaani kuna kawaida ya kusema kipi bora nimfunge yule ambaye amempa mtoto mimba au nimuache anilelee mtoto wangu na haya wanayafahamu”
Kaimu mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Njombe George Makacha ambaye ni mwanasheria na Valentino Hongoli ambaye ni mwenyekiti wa halmashauri hiyo wamewataka madiwani na maofisa watendaji kuitumia mikutano yao ya hadhara kuhakikisha wanatoa elimu ya kupinga ukatili wa kijinsia katika jamii.
“Sheria inataka kama motto amepewa mimba lazima sheria zichukuliwe na sisi kama viongozi ni vema tutoe elimu zaidi ili wazazi waelimike na kuona uchungu juu ya watoto”alisema George Makacha
Valentino Hongoli alisema “Wakati mwingine sisi wenyewe tukijitathmini utakuta viongozi,watendaji na baadhi ya wananchi wanaonekana kioo kwenye jamii utakuta ni watelekezaji”
Katika ripoti ya afisa ustawi wa jamii halmashauri hiyo kwa upande wa wanafunzi waliopata ujauzito ni 16 kwa mwaka 2020 na 18 kwa mwaka 2021.



Comments
Post a Comment