Watu saba wa familia moja katika mtaa wa Magomeni wilayani Ilemela mkoani Mwanza wamenusurika kifo baada ya nyumba yao kuteketea kwa moto ambao chanzo chake bado hakijajulikana.
Moto huo uliyozuka kuanzia saa 1:30 asubuhi umedumu kwa zaidi ya saa moja kabla ya kikosi cha Zimamoto na Uokoaji kufika na kuudhibiti huku samani zilizokuwa katika vyumba vitatu kati ya kumi vya nyumba hiyo zikiteketea.
Kijana wa familia hiyo, Emmanuel Ng'habi amesema hakuna majeruhi hakuna mtu aliyejeruhiwa katika familia hiyo zaidi ya samani zilizoteketea.
"Nawashukuru Zimamoto wamefika katika eneo la tukio kwa wakati na wametusaidia kudhibiti moto huu kwa wakati kabla haujasambaa katika nyumba za jirani," amesema Ng'habi.
Mpangaji katika nyumba hiyo, Veronica Jumanne amesema moto huo umeteketeza samani zote zilizokuwa katika chumba chake huku akitoa wito kwa Zimamoto kutoa elimu mara kwa mara ili kuinusuru jamii dhidi ya majanga hayo.
Askari wa zamu wa Zimamoto Wilaya ya Ilemela, Daudi Mboelwa amesema wanaendelea na uchunguzi kubaini chanzo cha moto huo.
"Tumefika hapa kwa wakati tukafanikiwa kuzima moto katika vyumba saba japo vitatu tumekuta vimeshateketea kwa moto, zaidi niwapongeze wananchi wa mtaa huu kwa ushirikiano wao ili kupambana na moto huu," amesema Mboelwa.
Comments
Post a Comment