TRW YASEMA UCHAGUZI MKUU MWAKA 2020 UMEZINGATIA KANUNI, SHERIA,HAKI,USAWA

 



TAASISI ya THE RIGHT WAY (TRW) ambayo ilikuwa inahusika na utoaji elimu ya Mpiga Kura na kutazama Uchaguzi Mkuu mwaka 2020 na kuhakikisha kuwa wa haki na usawa imesema Uchaguzi ulikuwa wa haki na usawa kwani wengi walifuata utaratibu uliowekwa bila kuvunja sheria.

TRW ilifanya utazamaji wa Uchaguzi Mkuu katika Mikoa 10 ya Tanzania Bara ambayo ni Dar es Salaam,Tanga,Simiyu,Mwanza,Katavi,Geita,Kilimanjaro,Arusha,Dodoma,Mtwara na Mbeya.

Akizungumza leo Oktoba 31,2020 jijini Dar es Salaam Mkurugenzi Mtendaji TRW Wallace Mayunga amefafanua kuhusu hali ya uchaguzi uliofanyika Oktoba 28,2020 ambapo ameeleza kwamba uchaguzi mkuu umefanyika na washiriki wote wameepuka hali ya rushwa na udanganyifu,kuna upatikanaji sawa wa rasilimali za taifa kwa wagombea wote wa vyama vyote vya siasa.

"Uchaguzi umefanyika katika mazingira ya amani na kwamba hakuna fujo wala vitisho, kuna fursa sawa za matumizi ya vyombo vya habari vya umma na binafsi kwa vyama vyote vya siasa pia kulikuwa na mazingira mazuri kwa wapiga kura kupata haki yao ya Kupiga kura hasa Tume imerahisisha kwa kuwepo kwa vituo vingi vya kupigia kura ili kila mmoja aweze kupata haki yake ya msingi,"amesema Mayunga.

Aidha Mayunga amesema pamoja na changamoto za rasilimali fedha lakini wameweza kuifikia mikoa 10 kwa kuweka watazamaji ambapo walifanya kazi hiyo na sasa wanaendelea kuwasilisha taarifa zao kwao ambazo zitasaidia katika kuandika taarifa yao kuu.

Pamoja na hayo Mayunga ametoa pongezi kwa Jeshi la Polisi na vyombo vya usalama kwani vimepiga hatua kuhakikisha usalama wa nchi na wapiga kura uliimarishwa kipindi chote cha Uchaguzi.Mkurugenzi Mtendaji TRW Wallace Mayunga akizungumza na Wanahabari leo jijini Dar,akielezea kuhusu utazamaji wa hali ya uchaguzi uliofanyika Oktoba 28,2020 na kufafanua zaidi kuwa uchaguzi mkuu umefanyika na washiriki wote wameepuka hali ya rushwa na udanganyifu sambamba na upatikanaji sawa wa rasilimali za taifa kwa wagombea wote wa vyama vyote vya siasa.

Afisa 'Programu',Uchaguzi na Elimu ya Mpiga kura kutoka taasisi ya THE RIGHT WAY (TRW),Ibrahim Samatta akizungumza mbele ya Waandishi wa Habari (hapo pichani) leo jijini Dar,akimkaribisha Mkurugenzi wa Tasisi hiyo kuzungumza na Wanahabari kuhusu hali ya uchaguzi uliofanyika Oktoba 28,2020 nchini.

Comments