Maonyesho Vyuo Vikuu yazaa neema kwa Wanafunzi 100 wa Ufamasia


CHUO Kikuu cha CT kilichoko katika mji wa Punjab nchini India kimetoa ufadhili wa nusu ada kwa wanafunzi 100 watanzania wanaotaka kusomea ufamasia kwenye chuo hicho.

Ofa hiyo ilitangazwa jana na Mkurugenzi wa  Idara ya Kimataifa ya chuo hicho,  Sourabh  Chaudhary.

Alikuwa akizungumza na wanafunzi na watu mbalimbali wanaotembelea maonyesho ya vyuo  vikuu yanayoendekea kwenye viwanja vya Mnazimmoja jijini Dar es Salaam.

Chuo hicho na vingine tisa vimekuja nchini kuonyesha kozi wanazotoa kwenye maonyesho hayo kwa mwamvuli wa wakala mkubwa wa elimu nje ya nchi, Global Education Link (GEL).

Alisema wanafunzi wote 100 watakaopenda kusoma fani hiyo kwenye chuo hicho  watapata punguzo Maalum(Scholarship) hadi 50% na utaratibu wa safari utakuwa mwezi huu wa nane.

Alisema kwa wanafunzi ambao bado wako kwenye mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) wao wataingia chuoni kuanzia mwezi wa Tisa.

Sourabh alisema urafiki kati ya Tanzania na India ni wa miaka mingi na kwamba serikali ya Tanzania imewekeza kwa kiasi kikubwa sana katika sekta ya afya hivyo ni dhahiri inahitaji wataalamu wa kutosha kuhudumia sekta hiyo.

Alisema pia serikali ya Tanzania imejitahidi

 kuboresha miundombinu kwa wanafunzi wa sayansi wakiwepo hao wanaotaka kusoma kozi za afya.

“Kwa kutumia urafiki baina ya nchi hizi mbili uongozi wa chuo umekubaliana ni vyema kuchagua kozi ambayo ina umuhimu na uhitaji mkubwa katika soko la ajira kwa  kuipunguzia gharama ili Watanzania wengi waweze kuisoma kwa maendeleo ya nchi na taifa kwa ujumla,” alisema

Aliwahakikishia wazazi kwamba kwamba wanafunzi kutoka Tanzania  huwa wanafanya vizuri sana kutokana na maandalizi mazuri yao katika elimu ya sekondari na wengi wao hupokea tuzo mbalimbali kutokana na umahiri wao wa kufanya vizuri,kujishirikisha na michezo na kuonesha tabia njema wawapo chuoni.

Alisema mbali na kozi hiyo ya famasia zipo kozi nyingi akitaja baadhi kuwa ni uhandisi, sanaaa na paramedics  na artificial intelligence kwa uchache.

 

Comments