Viongozi wa dini watakiwa kuzidi kuhamasisha wanaume kufanyiwa tohara


 


Na Amiri Kilagalila,Njombe.

Viongozi wa dini mkoani Njombe wametakiwa kuongeza nguvu katika kuhamasisha wananchi mkoani humo kufanya Tohara ili kujikinga na maambukizi ya virusi vya ukimwi.

Hayo yamesemwa na katibu tawala wa mkoa wa Njombe Judica Omary katika kikao cha wadau wa afya mkoani humo kilicholenga kuwajengea uwezo katika utekelezaji wake.


Alisema ufanyaji wa Tohara kwa wanaume una mchango mkubwa kiafya wa kuepuka magonjwa ya kuambukiza ikiwemo ukimwi.

Alisema kuna haja ya kuweka mikakati mahususi ambayo itasaidia kuikabili jamii ambayo haiamini kuhusu Tohara kwa kutoa elimu mara kwa mara.

"Nimefurahi kwamba uwakilishi wa viongozi katika taasisi za dini ni mkubwa kwakuwa naamini nyinyi mtakuwa na nafasi kubwa ya kuendeleza elimu hii nzuri" alisema Judica.

Mganga mkuu wa mkoa wa Njombe Dkt. Zabron Masatu alisema ili kufanikiwa katika zoezi hilo ushirikiano unahitajika baina ya maafisa afya, viongozi wa dini pamoja na serikali.

Alisema kama mkoa una kazi ya kufanya ili kuhakikisha kuwa  wananchi mkoani hapa wanapata huduma hiyo muhimu ya Tohara kinga.

"Kama ilivyo katika takwimu tuna asilimia 65.3 na mpaka sasa hivi kitaifa tuna asilimia 77.4 kwahiyo mpaka sasa hivi tupo chini kwa malengo ya kitaifa,tuna kazi ya kufanya kuhakikisha wananchi wetu wanaendelea kupata huduma ya tohara kinga"alisema Dkt Masatu.

Viongozi wa dini walioshiriki kikao hicho akiwemo shekhe wa mkoa wa Njombe Rajab Msigwa na mchungaji wa kanisa la KKKT Nelson Godiwe walisema tafiti nyingi kuhusu mambo ya Tohara za kiafya zina mlengo chanya ambao hauleti ukakasi katika kuelimisha jamii.

"Ukimuona nabii Ibrahim baba wa imani alifanyiwa Tohara akiwa mtu mzima mwenye umri wa miaka themanini maandiko yanaonyesha kwahiyo inawezekana" alisema Rajab.

Aidha wadau wengine wa afya wameshauri ushirikishwaji wa watoa huduma ngazi ya jamii.

“Kuna wazee wa mila na desturi na kama tutawahusisha wengi hili litafanikiwa”walisema wadau

Mpango huo umelenga kushawishi halmashauri kuongeza na kuvijengea uwezo vituo vya utoaji wa huduma za Tohara ambavyo kwasasa vipo kumi na sita kwa mkoa mzima wa Njombe.

Comments