Somo la Uchoraji kutarajiwa kuleta Mageuzi



KATIBU  Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar bwana Ali Khamis Juma amesema somo la sanaa ya uchoraji ( fine art) ni somo litakalo leta mageuzi ya sanaa katika sekta ya elimu.

Ameyasema hayo wakati alipozungumza wakati alipotembela darasa maalum la walimu wa somo la sanaa ya uchoraji (fine art) Katika Skuli ya Sekondari Mwanakwerekwe 'C' mjini Unguja.

Amesema muda umefika sasa kwa Walimu kuendelea kujiendeleza kwa kuanzisha fani zitakazoendelea kuleta mageuzi katika sekta ya elimu.

Amesema ni jambo la kupongezwa kuona Zanzibar inaanzisha somo la sanaa na kuendeleza darasa maalum la sanaa ya uchoraji fine art.

Amewanasihi walimu hao kuendelea kuwa na moyo wa kujitolea katika kuhakikisha sekta ya elimu inaendelea kufanya vizuri nchini.

Aidha amewasisitiza Walimu hao kutotosheka na taaluma hiyo bali wanafursa ya kuongeza ujuzi zaidi kwa lengo la kuendeleza somo hilo kwa kuibua vipaji mbalimbali katika jamii.

Amesema Wizara inategemea kufanya mageuzi makubwa katika sekta elimu ikiwa lengo ni kuifanya elimu iwe na hadhi huku somo hilo itahakikisha linapewa kipao mbele.

Hata hivyo bwana Ali amewanasihi walimu kuwa na moyo wa kizalendo kwa kurejea nchini mara baada ya kumaliza masomo hasa wale wanaopata fursa ya kwenda kusoma nje ya nchi yao.

Aidha amesema kazi ya ualimu ni kazi ngumu ambayo ni wito ambao unahitaji moyo, ujasiri na upendo, hivyo amesema taaluma zao wanazowapa Wanafunzi ni hakiba yao isiyoisha milele. 

Nae Mkurugenzi Idara ya Elimu Sekondari bi Asya Iddi Issa amesema Walimu wa somo la sanaa ya uchoraji (fine art) wanahitaji pongezi kwa uamuzi wao wa kuanzisha darasa la kuweza kuwaongezea ujuzi wao wenyewe na itapelekea kufanya kazi zao kwa kujiamini ikiwa ni jambo la kupigiwa mfano kuweza kujitoa kupata taaluma hiyo bila ya kuisubiri Wizara iwawezeshe.

Kwa upande wake Mkurugenzi Idara ya Mafunzo ya Ualimu bi Maimuna Fadhili Abasi amesema Idara yake ipo tayari kuhakikisha inatoa kipaombele kwa darasa hilo kwa kuwaandalia vyeti maalum vya kuhitimu mafunzo hayo chini ya usimamizi wa Wizara ya Elimu Zanzibar.

Jumla ya Walimu thalathini na mbili wamejitolea kupata taaluma zaidi ya somo la sanaa ya uchoraji (fine art) kutoka Skuli mbalimbali.

 

Comments