Walimu Masasi wanaowafungia wanafunzi darasani kwa kutotoa mchango wa chakula waonywa



Na Hamisi Nasri, Masasi

WALIMU wa shule za msingi za halmashauri ya mji Masasi mkoani Mtwara wamepewa onyo kali kuchana na tabia ya kuwafungia darasani wanafunzi ambao hawajachangia mchango wa chakula shuleni ili wasile chakula pindi wenzao waliochangia wanapokula.

Onyo hilo limetolewa jana mwenyekiti wa halmashauri ya mji Masasi kwa niaba ya madiwani wa halmashauri hiyo wakati wa kikao cha baraza la madiwani kilichoketi katika ukumbi wa halmashauri hiyo mjini Masasi.

Natumba alisema hivi sasa katika baadhi ya shule za msingi za halmashauri ya mji Masasi kumeibuka na tabia ya ukatili kwa wanafunzi wa shule za msingi hasa ambao wazazi na walezi hawajawachangia mchango wa chakula watoto wao shuleni.

Alisema baadhi ya walimu wamekuwa tabia ya kuwafungia wanafunzi darasani na komeo kisa wanafunzi hao hawajatoa mchango wa chakula shuleni hivyo muda unapofika wa kula chakula nyakati za mchana wanafungiwa ili wasije kula chakula ambacho wenzao wamechangia.

Namtumba alisema kitendo cha wanafunzi kufungiwa ndani ya darasa na komeo ili wasile chakula na hata kurudi nyumbani kwao kwenda kula chakula ni kitendo cha ukatili kama vitendo vingine vya ukatili wanavyofanyiwa watoto.

Mwenyikiti huyo alisema shule ambazo ndio vinara kwa walimu wake kufanya vitendo hivyo ambavyo ni ukatili kuwafungia darasani wanafunzi kwa komeo kwa sababu ya wazazi wao hawachangia chakula ni shule ya msingi Kambarage, Mkuti, Nyasa, Mtandi, Maendeleo na Kitunda shule ya msingi ya mfano.

 “Kuanzia leo tunapiga marufuku tabia hizi na kwamba tunatoa onyo kwa walimu wa shule hizi kuacha mara moja vitendo hivyo na mwalimu yoyote ambaye tutambaini akifanya kitendi kama hiki basi atachukuliwa na hatua.”alisema Namtumba

Namtumba alieleza kuwa kitendo cha wanafunzi kufungiwa darasani huku wakiwaangalia wenzao wanakula chakula alafu baadae wanafunzi hao wanachanganika darasani na wenzao ambao tayari wamekula chakula ni kwamba wale ambao hawajala hawawezi kusoma vizuri hivyo ni bora wale ambao hawajachangia chakula kuwaruhusu kwenda kwao kwa ajili ya kula.

Alisema walimu wa shule hizo wanahitaji kufahamu kuwa watoto ambao wazazi wao wameshindwa kutoa mchango wa chakula sio kama wamefanya hivyo makusudi bali kutokana na hali ya ugumu wa maisha na pia wapo ambao wanaishi karibu na shule hivyo kutoona umuhimu wa kuchangia chakula kwa watoto wao hivyo kwa sababu hiyo walimu wasiwahukumu wanafunzi hao.

Namtumba alisema mwanafunzi ambaye hajachangia mchango wa chakula shuleni pindi muda wa kula unapofika aruhusiwe kurudi nyumbani kuliko mwalimu kufanya maamuzi ya kumfungia darasani ili asile chakula au iwe kama njia ya wazazi na walezi kuhamasika kutoa mchango jambo hilo kwa sasa halitakiwi katika shule zote za halmashauri ya mji Masasi.

Naye diwani kata ya Nyasa, Mbaraka Kodo alisema walimu kama hao ambao wanafanya vitendo hivyo ni vema wakapewa adhabu kwa sababu huo ni ukatili kwa watoto na kwamba sifa hiyo ya walimu kuwafungia wanafunzi darasani na komeo ili wasile chakula na wanafunzi ambao wamechangia chakula imetawala katika shule za msingi za mji Masasi hivyo lazima vikomeshwe.

Kwa upande wake kaimu mkurugenzi wa halmashauri ya mji Masasi, Abirahi Mfinanga alisema amesikitishwa kusikia jambo hilo na anatoa wito kwa walimu ambao wanafanya vitendo hivyo kuacha mara moja iwapo vitendo hivyo vikiendelea adhabu kali itatolewa kwa walimu hao.

 

Comments