Samia: Tutatoa mwongozo ulipaji kodi na misamaha


 

Rais Samia Suluhu Hassan amesema Serikali inaandaa kitini ambacho kitatoa mwongozo wa jinsi mashirika yasiyo ya kiserikali yatakavyonufaika na misamaha ya kodi iliyopo kwa mujibu wa sheria.

Rais Samia ameyasema hayo leo Alhamisi Septemba 30, 2021 jijini Dodoma wakati wa mkutano mkuu wa Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (Nacongo) uliozikutanisha NGO zote zinazofanya kazi hapa nchini.

Kauli hiyo ya Rais Samia imetokana na maombi yaliyotolewa na Mwenyekiti wa Nacongo, Dk Lilian Badi wakati akiwasilisha risala yao kwa Rais Samia kwa kueleza changamoto mbalimbali zinazoyakabili mashirika yasiyo ya serikali.

Amebainisha changamoto hizo kuwa ni pamoja na kupatikanaji wa misamaha ya kodi kwa mashirika yasiyo ya serikali na changamoto ya upatikanaji na uhuishaji wa vibali vya ukaazi kwa raia wasio Watanzania.

“Changamoto hizi zikifanyiwa kazi zitasaidia mashirika yasiyo ya kiserikali kuweza kuchangia maendeleo kwa taifa kwa kushirikiana na serikali,” amesema Dk Badi ambaye alichaguliwa Julai mwaka huu kuwa mwenyekiti wa Nacongo.

Akizungumza katika mkutano huo, Rais Samia amezungumzia changamoto hizo akisema Serikali inaandaa kitini ambacho kitatoa mwongozo wa namna mashirika yasiyo ya kiserikali yatakavyonufaika na msamaha wa kodi ambayo baadhi yao wanastahili kupata.

“Tunafahamu kwamba kuna changamoto katika mifumo yetu ya kodi na pia zipo baadhi ya taasisi ambazo zinastahili kupata mikopo. Tumeanza kufanyia kazi masuala yote haya.

“Kuhusu msamaha wa kodi kwa mashirika yasiyo ya kiserikali ambayo yanafanya kazi kwa hisani, tayari tumekamilisha kuandaa kitini kinachotoa mwongozo wa namna mashirika yasiyo ya kiserikali yatanufaika na misamaha ya kodi. Tuko kwenye hatua za mwisho,” amesema.

Kuhusu changamoto ya upatikanaji wa vibali, Rais Samia amesema sasa kuna mfumo wa kielektroniki ambao umepunguza urasimu na vibali vinapatikana haraka ndani ya siku moja hadi tatu tofauti na ilivyokuwa zamani.

“Tangu Aprili 2021, uidara ya uhamiaji na idara ya kazi wameanzisha mfumo wa kielekroniki ambao umepunguza sana urasimu.

“Nimeambiwa kwa sasa endapo mwombaji atakuwa amekamilisha taratibu zote, anapata vibali katika kipindi cha siku moja hadi tatu kutoka siku 14 na zaidi zilizokuwa hapo nyuma. Hivyo kwa sasa kazi imebaki kwa waombaji kuwasilisha maombi yaliyokamilika,” amesema kiongozi huyo.

Kuhusu ucheleweshaji wa utoaji wa vibali vya utekelezaji wa miradi na afua mbalimbali, Rais Samia amesema; “natoa rai kwa mamlaka za serikali za mitaa kutoa ushirikiano wa kutosha kwa mashirika yasiyo ya kiserikali ili kwa pamoja tujenge nchi yetu.”

 

Comments