WHO: Ulaya bado inaandamwa na janga la Covid-19


 


Shirika la Afya ulimwenguni WHO limeripoti ongezeko la asilimia 7 ya maambukizi ya virusi vya corona barani Ulaya mnamo wiki iliyopita, eneo pekee duniani ambalo limeshuhudia kupanda kwa idadi ya visa vya maradhi hayo. 

Katika ripoti yake ya kila wiki iliyochapishwa jana WHO imesema wiki iliyopita kulikuwa na visa vipya milioni 2.7 vya Covid-19 na zaidi ya vifo 46,000 barani Ulaya, huku mataifa ya Uingereza, Urusi na Uturuki ndiyo yameshuhudia idadi kubwa ya visa vya maambukizi. 

Taarifa hiyo inaonesha kupungua kwa hadi zaidi ya asilimia 15 idadi ya visa vya Covid-19 barani Afrika na kwenye mataifa ya magharibi mwa bahari ya Pasifiki. 

Barani Afrika idadi ya vifo pia imepungua kwa karibu robo licha ya kanda hiyo kukabiliwa na upungufu mkubwa wa chanjo za virusi vya corona. 

Maeneo mengine ikiwemo kanda ya Amerika na mashariki ya kati yameshuhudia kiwango sawa cha maambukizi na vifo kama ilivyoripotiwa wiki iliyopita.


Comments