IGP Sirro awaonya wanaokata viungo binadamu, asema ni ushamba


 


Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania (IGP), Simon Sirro amesema yoyote atakayekutwa amekata kiungo cha binadamu mwenzake kwa lengo la kujipatia utajiri atamshughulikia kwa mujibu wa sheria akisema kufanya hivyo ni unyama na ushamba.


Ametoa onyo hilo leo Ijumaa Novemba 19, 2021 wakati wa ziara yake ya kukagua jengo la ofisi za Jeshi la Polisi zinazojengwa wilayani Lushoto Mkoani Tanga.


Kauli ya IGP Sirro imekuja siku chache baada ya tukio la kufukuliwa kwa maiti ya mtu mwenye ulemavu wa ngozi (albino) na kukatwa mguu na watu waliokamatwa na kukiri kufanya hivyo katika Halmashauri ya Bumbuli.


Amesema kuwa Jeshi la Polisi halina muhali na muhalifu wanaofanya matukio hayo kwani huo ni ushamba wakudanganywa na waganga wa kienyeji kuwa kupata utarijiri lazima ukate kiungo cha binadamu.


"Acheni kudanganywa na waganga wa kienyeji sababu mganga atakupaje utajiri wakati yeye mwenyewe ni masikini? nyumba anayokaa haieleweki na wala hajasomesha watoto wake " Amesema Mkuu huyo wa Jeshi la Polisi huku akisisitiza Jeshi hilo lina timu ya kupambana na mauaji ya aina zote 


Amesema mtu akipelekwa mahakamani kwa kosa hilo la kukata kiungo cha binadamu atanyongwa kwa kuwa mtu huyo ni mnyama hivyo lazima ashughulikiwe.


"Suala la kukata viungo unategemea kuwa tajiri vilishapitwa na wakati halafu ni ushamba, unakata mtu kiungo maana yake anakufa tukikukamata adhabu yake ni kunyongwa" amesema IGP Sirro


Amewaomba viongozi wa dini na wanasiasa kusaidi kutoa elimu kwa jamii ili waache na hizo Imani.


Akizungumzia hali ya amani, IGP Sirro amesema kwa Lushoto hali ni shwari tofauti na miaka ya nyuma ambapo kulikuwa na gaidi wa kutisha huku akisema waliokuwa wanajihusisha na ugaidi walikamatwa mlima Simba.


Naye Kamanda wa Polisi Mkaoni Tanga, Safia Jongo amesema kuwa Serikali imewapatia Sh250 milioni kwaajili ya ujenzi wa jengo hilo huku Jeshi hilo kupitia mfuko wake wa tuzo na tozo  imetoa Sh160  millioni japo fedha zilizokuwa zinahitaka  kwa ajili ya kukamilisha jengo hilo Sh500 milioni.


Kwa Upande wake Mkuu wa Wilaya ya Lushoto, Kalist Lazaro amehidi kutoa ushirikiano kuendeleza na ujenzi  wa jengo hilo ambalo litakuwa na ofisi  za utawala, kituo cha Polisi na upande wa upelelezi.


Mbunge wa Jimbo hilo, Shabani Shekilindi ‘Bosnia’ amechangia mifuko 50 ya saruji 50 huku kupitia Mfuko wa Jimbo amechangia Sh5 milioni.


Wengine waliochangia ujenzi huo ni Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ambayo imechangia mifuko 50 na mfanyabiashara Emanuel Mvungi amechangia mifuko 200ya saruji.


Katika hatua nyingine IGP Sirro ameonyesha kusikitishwa na nyumba za makazi ya Polisi zilizopo wilayani humo ambapo amesema mazingira hayaridhishi.


Amesema meahidi kupitia Mfuko wao wa Polisi kutoa Sh150 milioni ili ujenzi wa makazi ya polisi.

Comments