MKUU wa Mkoa wa Songwe Omary Mgumba amemwagiza Mkuu wa Wilaya ya Momba Faki Lulandala kuhakikisha anawachukulia hatua wazazi wote ambao wanawatumikisha watoto wao waliofikisha umri wa kuanza shule kuchunga mifugo.
Mkuu wa Mkoa wa Mkoa ametoa maagizo hayo katika mikutano ya hadhara na Wananchi wa kata ya Nzoka akiwa katika ziara ya siku tatu wilayani hapo akikagua miradi ya maendeleo na kuongea na Wananchi.
Alisema mzazi yeyote atakaye bainika kumpeleka mtoto wake kuchunga aliyetimiza umri wa kwenda shule atachukuliwa hatua kali za kisheria.
"Mtoto mdogo mwenye umri wa kwenda shule ya awali au Msingi kutumikishwa kwa kuchunga mifugo ni kuhujumu Taifa , mheshimiwa mkuu wa Wilaya simamia hili ,
Mtoto hata kama umemzaa wewe ni nyala ya Serikali , hivyo hatutavumilia vitendo hivyo ambavyo vimelalamikiwa na baadhi ya Wananchi wa kata hii ya Nzoka" alisema Mgumba.
Awali mkazi wa kata ya Nzoka Ruben Sinjele alimuomba mkuu wa Mkoa kukemea changamoto hiyo ya wazazi kupeleka watoto wao kuchunga mifugo badala ya kwenda shule.
Alisema wazazi wengi wamekuwa wakiwapeleka watoto wao kwenda kufanya vibarua vya kuchunga mifugo kwa wafugaji na kupelekea kukosa haki yao ya kupata elimu na ujinga kuongezeka .
Hivi karibuni Waziri wa mifugo na Uvuvi Mashimba Ndaki alisema kitendo Cha wafugaji kuwatumia watoto wadogo kuchunga ng'ombe hupelekea kuibuka kwa migogoro ya wakulima na wafugaji kutokana na kuzidiwa na mifugo.
Alisema mifugo ichungwe na watu wazima na sio watoto wadogo ambao inatakiwa wawe shule kupata haki yao ya Msingi.
Comments
Post a Comment