Mkenge, Mwakamo na Ridhiwani wapeta Ubunge

 

 

 


Na Omary Mngindo, Pwani.

WAGOMBEA Ubunge Jimbo la Bagamoyo Muharami Mkenge, Kibaha Vijijini Michael Mwakamo na Ridhiwani Kikwete Jimbo la Chalinze wametangazwa kuwa washindi katika majimbo yao.

Mkenge wa CCM ametangazwa mshindi na Msimamizi wa Uchaguzi Fatuma Latu, kwa kujinyakulia kura 23,159, Vitalis Maembe wa ACT Wazalendo kura 5,592, Emmanuel Mathayo wa CHADEMA kura 2,645 na Mohamed Mshamu wa CUF kura 692.

"Waliojiandikisha 109,091 waliopiga kura 33,044 kura halali 32,088 zilizokataa zilikuwa 956, zoezi limekwenda vizuri  changamoto iliyojitokeza ni kunyesha kwa mvua hali iliyosababisha baadhi ya maeneo miundombinu ya barabara yalikuwa yanapitika kwa shida," alisema Latu.

Jimbo la Chalinze Msimamizi Ramadhani Posi amesema kuwa  zimepigwa kura za Urais, na Madiwani Kata 6 kati ya 15 kutokana na mgombea Ubunge Ridhiwani Kikwete kupita pasipokuwa na mpinzani, huku Kata 9 nazo zikipita bila kupingwa.

"Kura zilizopigwa ni za Urais na Madiwani wa Kata 6 kati ya 15 zilizokuwepo jimboni kwetu, mgombea wa Ubunge Ridhiwani Kikwete na madiwani wa Kata 9 wamepita pasipokupingwa kutokanna na vyama vingine kutokuwa na wagombea," alisema Posi.

Kibaha Vijijini Msimamizi wa Uchaguzi jimboni humo Butamo Ndalahwa amemtanga Michael Mwakamo kuwa Mbunge Mteule kwa kujishindia kura 18,388, dhidi ya Edward Edmond wa CHADEMA kwa kura 5,083 huku Hamada Abdalahamani ACT Wazalendo akipata kura 465.

Wengine waliopata kura Kibaha Vijijini ni pamoja na Ezekiel Mbwambo wa CCK amejinyakulia kura 168, Selemani Mgonela wa CUF kura 219 wakati Mrisho Mkopi wa UPDP kura 62.

Jimbo la Kibaha Mji Maimamizi wa Uchaguzi Jenipha Omolo amemtangaza Silvestry Koka wa CCM kuwa mshindi kwa kura 29,797 dhidi ya12,234 za Michael Mtali wa CHADEMA.

Jimbo la Mafia Juma Kipanga wa CCM ameshinda kwa kura 12,691, Shahari Mngwali wa ACT Wazalendo 2,342 Zaituni Alli wa CUF 1759 na Ally Hassani wa CHADEMA kura 713.

Upande wa nafasi za Udiwani kwenye majimbo yaliyopo mkoani Pwani, mpaka sasa Kata ambayo tayari imethibitishwa kuchukuliwa na chama nje ya Chama Cha Mapinduzi CCM ni Kata ya Dutumi pekee iliyopo Jimbo la Kibaha Vijijini.

Mpaka kukamilika kwa mchakato mzima kuanzia kampeni mpaka kutangazwa kwa matokeo yake, hakujaripotiwa kutokea kwa fujo aina zozote ndani ya majimbo yaliyomo ndani ya Mkoa wa Pwani.


Comments