- Get link
- X
- Other Apps
“Kukata tamaa ni dhambi kubwa” ni kauli ya kujiamini ya Agness Mwita (16) si jina halisi.
Huyu ni binti aliyefaulu mtihani wa darasa la saba kwa daraja A, baada ya kuruka vikwazo vingi kutoka kwa mzazi wake aliyetaka aache shule ili akeketwe.
Mwanafunzi huyo anayeishi kituo cha Hope For Girls And Women Tanzania kilichoko Mugumu wilayani Serengeti, alikatishwa masomo akiwa darasa la pili ili akeketwe kisha aolewe, kutokana na mtazamo wa baba yake kuwa akimuoza atamletea ng’ombe.
Ilikuwaje
Huku akionyesha kusikitishwa na jinsi ndoto yake ilivyokuwa ikatishwe alisema akiwa darasa la pili katika Shule ya Msingi Kibeyo, baba yake mzazi alimkatisha masomo kwa madai kuwa anatakiwa kukeketwa kisha kuolewa kwa kuwa kwake watoto wa kike hawezi kuwasomesha.
“Mimi ni mtoto wa nne lakini ni wa kwanza kwa wasichana . Kaka zangu walikuwa wanasomeshwa mmoja chuo mwingine sekondari, nilipoambiwa hivyo niliumia sana nikamwambia bibi naye akaungana na baba kuwa natakiwa kuolewa.”
“Nilimwambia bibi kuwa siko tayari kukeketwa na kuolewa katika umri mdogo hivyo maana nilikuwa nishasikia madhara ya ukeketaji. Nilimweleza mama dhamira yangu ya kusoma na athari za ndoa za utotoni zinavyowatesa wanaoolewa,alinielewa lakini alipojaribu kumweleza baba alipigwa,” alisema.
Alilazimika kukaa nyumbani kazi yake ikawa ni kuchunga ng’ombe akisubiri kipindi cha kukeketwa hali ambayo ilimuumiza mdogo wake ambaye kila jioni wakiwa wamekaa alimweleza athari za ukeketaji kwa kuwa alikuwa kwenye klabu ya kupinga vitendo vya ukeketaji na akamwambia waliambiwa asiyetaka akimbilie ‘Nyumba Salama.’
Alivyokwepa kukeketwa
Mwaka 2016 wazazi wake wakiwa wamehamia kijiji cha Nyichoka watoto waliagizwa kwenda Kibeyo kwa bibi yao ili wakafanyiwe maandalizi ya kukeketwa,
“Wakati mama ananipangia nguo aliona nilivyokuwa na huzuni kubwa, ilimuumiza sana maana alijua ndoto yangu ya kusoma itakuwa imekufa kwa kuwa kilichokuwa kifuate ni kuolewa.”
Hata hivyo, aliamua kuvunja ukimya na kumwambia mama yake kuhusu mpango wake wa kukimbilia Nyumba Salama kutokana na maelekezo ya mdogo wake naye alimkubalia na kumwelekeza.
“Mama aliniambia nishukie shule ya Mapinduzi niulize Nyumba Salama nitampata Rhobi, kweli safari yangu iliishia hapo wengine wakaenda stendi nikamtafuta nikampata wakanipokea ndiyo ukawa mwanzo wa maisha mapya ya kuelekea kutimiza ndoto yangu ya kusoma,” alieleza.
Aanza shule
Alisema ilibidi apelekwe dawati la Jinsia la Polisi na kuhojiwa waliporidhika kuwa alikuwa kwenye hatari ya kukeketwa na hatimaye kuozwa, mratibu wa kituo alimuuliza kama yuko tayari kusoma, swali alilotegemea kwa kuwa ndiyo kiu yake.
“Nilipelekwa darasa la tatu shule ya Little Flower Mugumu nikasoma mwaka mmoja kisha nikaacha baada ya kutokea matatizo Kituo cha Nyumba Salama na mratibu akaanzisha kituo cha Hope tukaamia hapo akanitafutia mfadhili wa kunisomesha.”
“Nilipelekwa shule hiyo nikaanzia darasa la tano mwezi Julai, nilipata shida kwa kuwa walikuwa wanafundisha kwa Kiingereza kwa kuwa penye nia pana njia niliamua kukomaa sana kwenye majaribio nikawa wa 32 kati ya 66,”anasimulia.
Matokeo hayo yalimpa nguvu ya kusoma sana kwa kuwa ndiyo siri ya mafanikio, hali hiyo ikamafanya katika majaribio yaliyofuata awe wa sita na baada ya hapo akawa anakuwa kwenye nafasi tatu za juu.
“Nilikuwa mwanafunzi bora kwa masomo yote, nikatunukiwa vyeti siku ya mahafali mama alilia sana kwa uchungu kuona mafanikio yangu,maana waliyemuona hana maana anatajwa kuwa shujaa. Baba hakufika kwa kuwa alishanilaani kuwa mimi si mwanawe kwa kuwa nilikataa kukeketwa,”anasema huku akifuta machozi.
Ndoto yake ni kuwa rubani
Agness anasema safari ya kuelekea kutimiza ndoto yake ya kuwa rubani inanukia, maana anaamini kwa ufaulu wake anakwenda sekondari na kama watu waliomsaidia wakiendelea kumshika mkono siku moja atakuwa mfano.
“Madaktari na manesi wanawake ni wengi lakini marubani ni wachache; nataka siku moja niwe angani na kumdhihirishia baba na wazazi wenye mitazamo kama yake kuwa mtoto wa kike ana thamani kubwa akiendelezwa na huo utakuwa mwisho wa laana yake maana nitakuwa mtu wa thamani ndani ya familia”anasema.
Azungumzia ukeketaji
Anasema athari za ukeketaji ni nyingi ukiacha za kiafya ni chanzo cha umaskini kwa baadhi ya familia.
‘‘Wanakeketa watoto na kuwaoza hawana uwezo wa kupambana na changamoto za maisha, wanazaa watoto katika umri mdogo hawawasomeshi na wanakuwa wakirithi tabia za kuwaoza’ huo ni umaskini mkubwa kwenye jamii,’’ anasema.
Rhobi Samwel ambaye ni Mkurugenzi wa shirika la Hope For Girls And Women Tanzania anasema ukatili wa kijinsia unaathiri maisha ya watoto wa kike
”Watoto wanaokimbilia kwetu mbali na kuwasaidia kisaikolojia, tunawaendeleza kielimu maana ndiyo msingi wa maisha yao,”anasema.
Anasema wakati wa likizo ya corona wazazi wengi waliitumia kuwakeketa watoto wao badala ya kuwatafutia masomo ya ziada na zaidi ya 60 walihifadhiwa kituoni hapo kabla hawajakeketwa na watano walikutwa wameshakeketwa.
Comments
Post a Comment