Waziri Jafo akoshwa na ujenzi wa vituo vya afya Njombe mjini,aagiza kimoja kupata vifaa tiba

 

 


Na Amiri Kikagalila,Njombe

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Selemani Jafo amefurahishwa na ujenzi wa vituo vya afya Kifanya na Makowo ambapo asilimia kubwa ya ujenzi wa vituo hivyo unatekelezwa kutokana na makusanyo ya mapato ya ndani na nguvu za Wananchi ambapo zaidi ya Shilingi  milioni mia saba za mapato ya ndani zimepelekwa kwenye vituo hivyo.

Aidha amemuagiza katibu mkuu wa wizara hiyo kuhakikisha kituo cha afya Kifanya kilichopo halmashauri ya mji Njombe kinapata vifaa ili kiweze kuanza kutumika

Akizungumza Mara baada ya kukagua shughuli za Ujenzi Katika Kituo cha afya kifanya ambapo Mhe.Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli alikipatia kituo hicho kiasi cha Shilingi Milioni kumi kusaidia ujenzi, Waziri Jafo amesema kuwa jitihada zilizofanyika kupitia makusanyo ya mapato ya ndani kwa kujenga vituo vya afya viwili ni kubwa na amezitaka Halmashauri nyingine kuiga Mfano huo.

“Kituo ni kizuri na Kimejengwa kwa mapato ya ndani.Tunavyozungumza juu ya vituo vya afya 487 sasa tunakwenda mpaka vituo mia tano. Ninyi Mko vizuri. Niwapongeze kwa kazi kubwa mliyofanya Mimi nimeona kuwa mnafanya kazi nzuri endeleeni na kasi hii. Majengo haya yanakwenda kuwahudumia Wananchi .Hata ukienda kukusanya ushuru Mwananchi anakuelewa. Sio unakwenda kukusanya ushuru lakini matokeo yake hayaonekani.Naomba niwapongeze. Mnyonge Mnyongeni lakini Haki yake mpeni”Alisema Waziri Jafo.

Jafo anaendelea kusema licha ya kuwepo na kasi ya ujenzi Vituo vya Afya Serikali  pia imeendelea kutoa ajira kwa Wataalamu wa Sekta hiyo ili kuhakikisha kuwa vituo hivyo vinafanya kazi na kutoa huduma iliyo bora ambapo zaidi ya Wataalamu wa Afya elfu kumi na mbili (12,000)waliweza kuajiriwa.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Njombe Mjini Deo Mwanyika na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Njombe Illuminatha Mwenda  wamemshukuru Waziri Jafo kwa kuweza kukagua ujenzi wa kituo hicho ambapo katika ziara hiyo ameweza kufanya mawasiliano na Katibu Mkuu TAMISEMI ili kuweza kupata vifaa  katika kituo hicho.

“Mheshimiwa Rais alituchangia milioni 10, Wananchi Wamechangia milioni 28 Halmashauri ya Mji Njombe imechangia milioni 370 ambapo sasa tupo katika hatua za mwisho za umaliziaji. Makadirio yetu ni milioni 420 kukamilisha ujenzi ambao utakuwa msaada mkubwa kwa Wakazi wa ene la Kifanya na maeneo ya jirani.”Alisema Mwenda.

Naye Mbunge wa Jimbo la Njombe Mjini Deo Mwanyika anasema”Mheshimiwa Jafo ametutia moyo sana nilimweleza juu ya uwepo wa vituo vya Afya viwili Kifanya na Makowo.Tumemwomba Vifaa. wakati wa Kampeni niliwaambia Wananchi Serikali imejenga kituo cha Afya na tutahakikisha kuwa kinapata vifaa na Wataalamu wakutosha na tumepata majibu ya vifaa. Tunashukuru sana.Wananchi wa Kifanya watambue sasa Serikali yao ipo kazini.”

Awali katika ziara hiyo Mheshimiwa Jafo alipata nafasi ya kuzungumza na Watumishi kutoka katika Halmashauri ya Mji Njombe ambapo amesisitiza suala la ukusanyaji mapato na kufanya matumizi sahihi na amewataka wakurugenzi wote Nchini kuhakikisha kuwa ifikapo Mwishoni mwa mwezi Desemba Halmashauri zote 185 ziwe zimekusanya zaidi ya asilimia 50 ya lengo ambapo tarehe 15 Januari atatoa taarifa ya ukusanyaji mapato kwa kila Halmashauri  kwa kipindi cha miezi sita. Pia amewataka Wakurugenzi kuhakikisha kuwa fedha zilizotolewa kwa ajili ya miradi ya elimu madarasa na mabweni ifikapo tarehe 30 Desemba miradi iwe imekamilika.

Comments