Diamond amtaja Baba yake mzazi

 

   


MSANII nyota wa Bongo Fleva, Naseeb Abdul almaarufu Diamond Platnumz kwa mara ya kwanza amefunguka kuhusu baba yake halisi na kueleza kwamba tangu mwaka 2000, ndipo alipojua kwamba baba yake mzazi ni Salum Idd Nyange na si Abdul Juma kama wengi walivyokuwa wakijua.

Diamond ameyasema hayo wakati akihojiwa katika kipindi cha The Switch kinachoruka kupitia kituo cha Redio cha Wasafi FM na kuongeza kuwa dada wa mama yake, ambaye pia ni mama mzazi wa ndugu yake, Rommy Jones (RJ) ndiye aliyemfanya aujue ukweli huo.

“… Wakati mimi nakua nilikuwa nikiamini mzee Abdul ndiyo baba yangu, kufikia mwaka 2000 nadhani, sikumbuki vizuri, ndiyo nikaja kuujua ukweli. Nakumbuka aliniambia mama yake RJ (Rommy Jonnes), ujue mimi nilikuwa ni mtu ambaye nina mapenzi sana na baba yangu, kipindi hicho najua ni mzee Abdul.

“Basi mama yake RJ akaniambia nenda pale Tandale Sokoni, muulizie mtu anaitwa Salum Bubu… ukifika pale mwambie mimi ni mwanao, basi nikatoka nikaenda na baada ya kufika pale, nikakutanishwa naye maana alikuwa anauza mchele kwa jumla.

“Basi baada ya kufika pale, watu wanaomjua wakawa wanaitana, ‘njoo umuone mtoto wa Salum’, basi nikakutanishwa naye, nikamwambia mimi nimetumwa hapa nije kukutafuta wewe, mimi ni mwanao, basi akanipa mchele na shilingi mia mbili,” amesema Diamond.

Anazidi kueleza kuwa baada ya miaka mingi kupita, takribani miezi minne iliyopita, alimuuliza tena mama yake, Sandra Kassim almaarufu Sanura au Mama Mondi ambaye alimthibitishia kwamba baba yake mzazi ni marehemu Mzee Salum Idd Nyange.

Alichokisema Diamond wakati wa mahojiano:-

“Ni kweli Mzee Abdul si baba yangu mzazi, Lakini tangu mtoto nilikua nampenda sana . Mpaka Mwaka 2000 ndio Mama yake @romyjons akaniambia ukweli ..

“Hakuna mtu ambae alikua anajua ukweli kwa sababu ndugu zangu wote niliwakusanya kwa upendo, kuanzia wakina Ricardo na Queen Darlin

“Hata baada ya kujua ukweli bado mapenzi yangu makubwa yalibaki kwa Mzee Abdul kama baba yangu.

Kwa bahati mbaya yeye aliniweka mbali sana, na nadhani kuna kipindi mama yangu alichukia kitendo cha yeye kusema kwenye vyombo vya habari kuwa simsaidii lakini kiukweli nimekua namsaidia,” anasema Diamond

Comments