Guinea yashuhudia vifo vya kwanza vya Ebola tangu mwaka 2016

   

 


Waziri wa afya nchini Guinea Remy Lamah amesema watu wanne wamefariki nchini humo kutokana na ugonjwa wa Ebola uliozuka baada ya miaka mitano. 


Lamah ameliambia shirika la habari la AFP kwamba wana wasiwasi kuhusu vifo hivyo vya kwanza tangu mripuko wa kati ya mwaka 2013-2016 ulioanzia nchini humo na kusababisha vifo vya watu 11300 katika kanda ya Afrika Magharibi. 


Mkuu wa taasisi ya taifa ya usalama wa afya Sakoba Keita, amewaambia wanahabari nchini humo kwamba muhanga wa hivi karibuni zaidi alikuwa muuguzi aliyeanza kuugua mwishoni mwa mwezi Januari na kuzikwa Februari 1. 


Baadhi ya wale walioshiriki katika mazishi yake, wanane walionyesha dalili za kuharisha, kutapika na kutokwa na damu. Watatu kati yao walifariki huku wanne wakiwa wamelazwa hospitalini.


Shirika la afya duniani WHO limekuwa likifuatilia kila mripuko mpya kwa uangalifu mkubwa tangu mwaka 2016 na kuutaja mripuko wa hivi karibuni zaidi katika Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo kama dharura ya kimataifa ya afya.

Comments