Kufuatia kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Chelsea, kocha wa Tottenham Hotspurs alia na majeruhi

   


Kufuatia kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Chelsea usiku wa jana kwenye EPL, kocha wa Tottenham Hotspurs, Jose Mourinho amesema kukosa baadhi ya wachezaji wake tegemezi wa kikosi cha kwanza kutokana na majeraha na wengine kuwa na uchovu ndiyo sababu kubwa zinazopelekea kuboronga.

Bao lililofungwa na kiungo wa Chelsea, Jorginho kwa mkwaju wa penalti dakika ya 24 baada ya mlinzi wa Spurs, Erick Dier kumkwatua mshambuliaji wa Chelsea Timo Werner, limewafanya masharobaro hao wa london kufungwa michezo mitatu mfululizo ya EPL kwa mara ya kwanza tokea Novemba 2012

Akijibia swali la kwanini Spurs haifungi mabao na kupata matokeo mazuri hivi sasa, Mourinho amesema “Sergio Reguilon, Harry Kane, Giovani Lo Celso na Delle Ali wanakosekana kwasababu ya majeraha, watu ambao wana maana kubwa sana kwenye namba yetu ya kushambulia”.

“Pia kukosekana kwao, kuna maana hatuna kikosi kipana kuweza kuzungusha wachezaji na wachezaji wengi tuliomaliza nao msimu jana wana uchovu mkubwa kutokana na mfululizo wa michezo wakati hatukuwa na wachezaji wengine wakuwapumzisha”.

Mourinho amesema pia kikosi hicho kinapitia wakati mgumu kutokana na wachezaji wake wengi uwezo wao wakujiamini umeshuka hivyo ana kazi ya ziada ya kufanya ili kurudisha ari na kujiamini kwao ili warudi kwenye njia zao za ushindi.

Licha ya kuboronga huko, Mourinho ameonesha kujivunia na upambanaji na umoja wa wachezaji wake kwenye mchezo wa Chelsea hususani kipindi cha pili cha mchezo.

Kipigo hiko kimemfanya Mourinho kuweka rekodi ya kupoteza michezo miwili mfululizo ya EPL kwenye dimba lake la nyumbani kwa mara ya kwanza tokea awe kocha lakini pia kushindwa kuifunga Chelsea katika michezo 7 ya mwisho, ameambulia sare 3 na vipigo 4.

Spurs imeshuka hadi nafasi ya 8 wakisaliwa na alama zao 33 licha ya kuwa nyuma na michezo 21, mchezo mmoja nyuma ya wapinzake wake anaowania nao nafasi nne za juu ilhali Chelsea imepanda hadi nafasi ya 6 wakiwa na alama 36 baada ya kucheza michezo 22.

Kwa upande mwingine, Kocha wa Chelsea, Thomas Tuchel ameweka rekodi ya kuwa kocha wa kwanza wa Chelsea kucheza michezo mitatu ya mwanzo bila kuruhusu bao rekodi ambayo iliwekwa mwaka 2004 na aliyekuwa kocha wa timu hiyo kwa wakati huo Jose Mourinho.

Comments