Mmishonari aliyetoroka Kenya ahukumiwa miaka 15 kwa unyanyasaji wa kingono

   


Mmishonari mkristo wa Marekani amehukumiwa kifungo cha zaidi ya miaka 15 gerezani kwa makosa yaunyanyasaji wa kingono dhidi ya wasichana wadogo katika kituo cha watoto yatima cha Bomet alichokuwa akiendesha pamoja na mke wake.

Gregory Dow, 61, alikubali kutekeleza makosa hayo ya uhalifu wakati kesi hiyo inasikilizwa katika jimbo la Pennsylvania.

Mashitaka dhidi ya Bwana Dow yalieleza kuwa alipoanza kunyanyasa wasichana wadogo, wawili kati yao walikuwa na umri wa miaka 11 na 12 huku mwingine akiwa na umri wa miaka 13.

Bwana Dow “alijifanya kuwa Mkiristo mmishonari ambaye angetunza watoto hao waliokuwa yatima,” Mwendesha mashtaka wa Marekani ameiambia mahakama. “Walimuita ‘baba'.

Lakini badala ya kuwa baba kwao, aliwanyanyasa ujana wao na kutumia hali yao ya uhitaji vibaya.”

“Alitumia nguvu na kushurutisha watoto kutekeleza vitendo hivyo vya vya kikatili na uhalifu, alinyemelea wasichana wadogo waliokuwa na uhitaji kwa kujifurahisha kingono,” waendesha mashtaka walisema.

Kituo cha watoto yatima cha Dow huko Boito, kilianzishwa mwaka 2008, na kufungwa mwaka 2017.

Mwaka 2008, Dow alianzisha makao ya watoto yatima magharibi mwa Kenya.

Makao hayo pia yalikuwa yanasimamiwa kwa pamoja na makanisa kaunti ya Lancaster jimbo la Pennsylvania, nchini Marekani kulingana na gazeti la eneo la LNP.

Shirika la Upelelezi Marekani- FBI na mamlaka ya Kenya zilimchunguza mtuhumiwa na akafikishwa mahakamani nchini Marekani.

"Mshtakiwa alijifanya kuwa Mmishonari Mkristo aliyejali watoto hao na kuwataka wamuite 'Baba'.

Hata hivyo, badala ya kuchukuwa majukumu ya baba, aliwanyanyasa ujana wao na kutumia vibaya hali yao ya kutojiweza," imesema Idara ya Sheria ya Marekani katika taarifa yake.

Alitoroka Kenya, Septemba 2017 baada ya kuibuka kwa madai ya unyanyasaji, taarifa hiyo imeongeza.

Pia inaendelea kusema kwamba Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI) lilichukua hatua baada ya kudokezwa tuhuma za mshtakiwa na Bwana Dow akashtakiwa Julai 2019.

"Gregory Dow kwa upande mwingine, alificha uovu aliokuwa nao katika imani yake, akiwa na matumaini kwamba nchini Marekani hakuna atakayejua anachofanya au kutunza watoto aliowanyanyasa. Alifanya makosa," Wakili William McSwain wa Marekani alisema.


Comments