RUWASA Kibaha yawahakikisha maji wakazi wa Ruvu

 


Na Omary Mngindo, Ruvu

WAKALA wa Maji na Usafi wa Mazingira Halmashauri ya Kibaha (Kibaha Vijijini) Mkoa wa Pwani, imewahakikishia wakazi wa Ruvu Minazi Mikinda kwamba watapata maji safi na salama.

Meneja wa Wakala hao wilayani hapa Debora Kanyika aliyasema hayo kijijini hapo, mbele ya Mbunge wa Jimbo Michael Mwakamo ambapo alisema kwa mwaka wa fedha 2020/2021 wameanza ujenzi wa mradi wa maji kijijini hapo.

Alisema kwamba mradi huo unahusisha ujenzi wa tanki la lita 100,000 kwenye mhimili wa mita 12 na vituo 14 vya kuchotea maji, mtandao wa Maji wenye urefu wa kilometa 8.5 kwa gharama ya shilingi millioni 269.

"Huu mradi tunataraji kuumaliza mapema sana, kaulimbiu yetu inasema Ruwasa maji bombani, maji bombani Ruwasa, niwaahidi wakazi wa Ruvu Minazi kuwa Serikali yetu chini ya Rais Dkt. John Magufuli imedhamiria kumtua mama ndoo kichwani," alisema Debora.

Awali Mbunge Mwakamo aliupongeza uongozi wa Ruwasa kwa juhudi hizo, huku akishauri wautumie mto Ruvu uliopo mita chache kutoka kulikojengwa tenki, ukilinganisha na kwenye chanzo wanachotaka kukitumia kuchukulia maji.

"Binafsi niliona hapa na chanzo cha mto Ruvu ni karibu, pia kuna maji yenye uhakika wa kipindi kirefu ukilinganisha na tunakotaka kuyachukua, isitoshe itatugharimu madawa mengi kuyatibu kutokana na maji yenyewe kuwa ya kisima ukilinganisha na ya mto Ruvu," alisema Mwakamo.

Kwa upande wao mmoja wa wakazi alisema kuwa mradi huo unataraji kuwaokoa kwenda kwenye mto Ruvu, ambako wanakabiliwa na changamoto ya mamba, hivyo mradi utakwenda kuwaondolea adha hiyo.

"Tunauomba uongozi wa RUWASA kuangalia uwezekano wa kuchuku maji katika chanzo cha mto Ruvu ambao upo karibu, pia maji yake yanadumu kwa muda mrefu tofauti na ya kisima, ambapo kuna yanakauka kipindi cha kiangazi kikali," alisema mkazi hiyo.

Comments