Wizara ya Maji yajipanga kumaliza tatizo la maji

  


Na Ezekiel Mtonyole - Dodoma.

Wizara ya maji imejipanga kukikisha inamaliza tatizo la maji katika maeneo mbalimbali ikiwamo kuwekeza nguvu nyingi katika utafiti wa vyanzo vya maji vya uhakika ili miradi ya maji iweze kutoa maji ya uhakika pindi inapokamilika.

Hayo yamebainishwa Wilayani Bahi Mkoani Dodoma na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya maji Mhandisi Nadhifa Kemikimba wakati wa maadhimisho ya siku ya wanawake Duniani ambapo katika Mkoa wa Dodoma yamefanyika katika Wilaya ya Bahi.

Amesema Serikali imedhamilia kumtua mwanamke ndoo kichwa kwa kuwekeza nguvu nyingi kuhakikisha inaondoa tatizo la maji ambapo mara nyingi humuathiri mwanamke katika kutafuta huduma hiyo.

"Serikali katika kuhakikisha inatatua tatizo la maji ndio maana tumeanzisha RUWASA hii inafanyakazi hadi ngazi za Wilaya na huko tunahakikisha wanataarifa Wilaya inavijiji vingapi na vingapi vinahuduma ya maji na vingapi hazina" amesema.

Amesema wamejikita kutafuta vyanzo vya maji vya uhakika ili miradi inayotekelezwa iwe ya uhakika na wananchi waweze kupata huduma ya uhakika ya maji katika maeneo yao.

" jana nilikuwa kigoma yote ni kuhakikisha haya niliyosema tupo kazini mda wote kuhakikisha tunamtua ndoo kichwani mwanamke nimefika katika kijiji nikauliza wenyeji wa eneo hilo vipi hali ya maji katika chanzo hiki, wakasema hapa maji uhakika mwaka mzima, sasa ni wakati wa wataalamu wetu sasa kuanza kutekeleza" amesema.

Amesema malengo yao ifikapo 2025 asilimia 95 ya watu waishio mijini wawe wanapata huduma ya maji safi na asilimia 85 ya watu wa vijijini wawe wanapata huduma ya maji safi.

Amesema kwa upande wa Bahi tayari wameanza kuchimba visima viwili vikubwa ambavyo wanauhakika vikianza kutoa maji na yakaingizwa katika mfumo yatapunguza uhaba wa maji katika Wilaya ya Bahi.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Bahi ambaye pia alikuwa mgeni rasmi katika maadhimisho hayo Mwanahamisi Munkunda amesisitiza kwa wanawake wanaopata nafasi za uongozi kuzitumia vizuri na kuwa chachu kwa wanawake wengine.

Amewaasa wanawake waliokatika nafasi za uongozi waache kujirahisisha na wawe na msimamo katika kutekeleza majukumu yao ya kazi, pia amewataka kusimamia maadili ya watoto kwani wao ndio wenye majukumu ya malezi.

"Ukiona familia imesimama na watoto wana maadili mazuri ujue kuna mwanamke kasimama imara na kuna mchango wake" amesema.

Amesema kuna haja ya wanawake hapa nchini kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli kwa kuwapa nafasi nyingi wanawake tofauti na miaka ya nyuma ambapo kwasasa wana Makamu wa Rais mwanamke.

Comments