Wizara yabaini ubadhirifu wa mabilioni ya dawa

  

 


Wizara ya Afya imebaini upotevu wa Sh26.7 bilioni za dawa uliosababishwa na uzembe, kutojali katika usimamizi wa mfumo wa ugavi wa bidhaa za afya, viashiria vya hujuma, wizi na udokozi wa bidhaa za dawa.


Hayo yamesemwa leo Machi Mosi, 2020 na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dk Doroth Gwajima wakati akitoa tamko kwa vyombo vya habari kuhusu matokeo ya ufuatiliaji huo.


“Nimekuwa nikipokea malalamiko mengi kutoka kwa wananchi kuhusu kukosa huduma ya dawa na vipimo katika vituo vya kutolea huduma katika ngazi zote kinyume na matarajio, jumla ya thamani ya fedha ambayo imethaminishwa kwa upungufu huu inakadiriwa kuwa siyo chini ya  Sh26.7 kwa kipindi cha Julai 2019 hadi Desemba 2020,” amesema Dk Gwajima.


Amesema kufuatia malalamiko hayo, wizara iliunda kamati ya wataalamu kutoka Wizara na taasisi za sekta mbalimbali ili kufanya ufuatiliaji katika hospitali 28 za rufaa za mikoa  kwa kipindi cha miezi 18.


“Lengo ilikuwa kubaini changamoto zinazochangia upatikanaji duni wa dawa na vipimo licha ya kuongezeka kwa mtaji wa dawa,


Jumla ya bidhaa za dawa na vipimo 20 hadi 30 tu kati ya nyingi zilizo kwenye orodha ya bidhaa za afya kwa kituo husika ndiyo zilifanyiwa ufuatiliaji kuanzia ununuzi, mapokezi na matumizi,” amesema Dk Gwajima.

Comments