AS Vita yaachana na Ibenge


Klabu ya AS Vita ya DR Congo imethibitisha kuwa imeachana na kocha wao wa muda mrefu Florent Ibenge mwenye umri wa miaka 59.

Rais wa Klabu hiyo Bestine Kazadi ametibitisha kuachana na Kocha huyo kwa kuwaambia wanachama na mashabiki wao kuwa wamefikia makubaliano na wanamshukuru kwa utumishi wake huku wakimtakia kila la kheri katika maisha yake.

''Ndugu mashabiki, ninatangaza kuondoka kwa kocha wetu Jean-Florent.Kwa niaba ya Klabu tunashukuru kwa utumishi wake na tunamtakia kila la kheri''Bestine Kazadi Rais wa AS Vita amesema..

Kocha huyo ambaye amedumu na klabu hiyo kwa miaka tisa, aliisaidia AS Vita kufika Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2014 na ile ya Kombe la Shirikisho ingawa mara zote alipoteza.

Mapema mwaka huu alihusishwa na kutua katika klabu ya Simba ya Dar es salaam baada ya kuonekana akifanya mazungumzo  na Mtendaji Mkuu wa Wekundu wa Msimbazi, Barbra Gonzalez lakini haikuwa hivyo.

Zipo tetesi zinazoainisha kuwa huenda uzembe wa benchi zima la ufundi la klabu hiyo chini yake ndilo lililopelekea AS Vita kupokonywa alama kwa kumchezesha mchezaji asiye stahili hali iliyopelekea washindwe kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya nchini Congo kwa kukatwa alama.

Comments