Putin ashutumu mitandao ya kijamii kupuuza sheria za Urusi


 


Rais wa Urusi Valdmir Putin ameituhumu mitandao ya kijamii ya nchi za Magharibi kwa kupuuza maombi ya maafisa wa Urusi kufuta ujumbe wenye maudhui haramu, lakini akasisitiza kuwa nchi hiyo haina mipango ya kuzuia kazi za mitandao hiyo. 

Serikali ya Urusi katika miezi ya karibuni imekuwa ikifanya upelelezi na kubana tovuti kama vile Facebook, Twitter na YouTube kwa kuweka maudhui yanayomuunga mkono mkosoaji wa utawala wa Kremlin Alexei Navalny. 

Akizungumza kwenye tukio la kila mwaka ya kujibu maswali ya umma kupitia televisheni, Putin amesema Urusi haitaifunga mitandao hiyo na badala yake itashirikiana nayo ili kufanya kazi kwa pamoja. Amesema hata hivyo mitandao hiyo inapaswa kuheshimu sheria za Urusi. 

Wakosoaji wa Ikulu ya Kremlin wanaituhumu serikali ya Urusi kwa kutumia kisingizio cha kuwalinda watoto wadogo na kupambana na itikadi kali kubana zaidi mitandao nchini Urusi, na kutengeneza kile kinachofahamika kama intaneti huru.


Comments