Saudi Arabia yapanga kuzidua shirika la pili la usafiri wa ndege


 


Mrithi wa kiti cha Ufalme wa Saudi Arabia Mohammed bin Salman ametangaza mipango ya kuzindua shirika la pili la kitaifa la usafiri wa ndege, kama sehemu ya mkakati mpana wa kuugeuza ufalme huo kuwa kituo cha kimataifa cha usafiri wakati ukitafuta kubadilika na kuondokana na utegemezi wa sekta ya mafuta. 

Uundwaji wa shirika la pili la ndege utaifanya Saudi Arabia kuwa taifa la tano duniani katika muktadha wa usafiri wa angani, kwa mujibu wa vyombo vya habari vya serikali, ambavyo hata hivyo havikutoa ufafanuzi zaidi juu ya lini na namna gani shirika hilo jipya litaundwa. 

Mwanamfalme Salman amekuwa akiongoza juhudi kwa Saudi Arabia, ambalo ndilo taifa kubwa zaidi kiuchumi la Kiarabu na nchi kubwa zaidi kijiografia katika kanda ya Ghuba, kuimarisha mapato yatokanayo na vyanzo visivyo vya mafuta kwa hadi dola bilioni 12 kufikia mwaka 2030. 

Shirika la habari la Saudia SPA, limesema kuifanya nchi hiyo kuwa kitivo cha usafiri wa kimataifa ambako kunahusisha ujenzi wa bandari, mitandao ya reli na barabara, kutaongeza mchango wa sekta ya usafiri kwa pato jumla la ndani kutoka asilimia 6 hadi 10.

Comments