Bibi Iluminata Mosha aliyefariki dunia akiwa na miaka 106 huenda akaweka historia ya kufa akiwa na umri mkubwa zaidi nchini Tanzania na nchi za Afrika Mashariki.
Bibi huyo ambaye ni mkazi wa kijiji cha Ruwa, kata ya Kilema Kaskazini, Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro alizaliwa mwaka 1915 kijijini hapo ambapo alibahatika kuwa na watoto 11 ambapo mpaka sasa walio hai ni 6.
Iluminata aliyefariki dunia Julai 27 mwaka huu amezikwa kijiji kwao leo Julai 31 ambapo wajukuu na vitukuu vyake wamejikuta wakicheza Sebene huku tarumbeta zikipigwa ikiwa ni Ishara ya kusherekea umri mkubwa alioishi hapa duniani.
Akisoma historia ya Marehemu, mjukuu wa bibi huyo, Bahati Mosha amesema ameacha vitukuu 42, wajukuu 24 na watoto 6 ambao baadhi yao ni madaktari, wahasibu na wahandisi.
Mwaka 2019 bibi huyo wakati alipofanya mahojiano na Mwananchi hili alieleza sababu za yeye kuishi miaka mingi huku akisema mfumo wao wa maisha ya zamani ni tofauti na sasa ambapo alidai wao walikuwa hawali vyakula vya viwandani hivyo magonjwa kama saratani na shinikizo la damu yalikuwa hayapo kama sasa.
“Hivi vyakula vya kisasa tulikua hatuli kabisaa na hata mafuta ya kupikia tulikua tukitumia mafuta ya asili ambayo yanatokana na wanyama, kama vile mafuta ya ngo’mbe, ndio maana zamani tulikua hatuumwi ovyo tulikua tukila vyakula vya asili, maradhi kama shinikizo la damu, kisukari, saratani yalikua hayapo kabisa ndio maana tumeweza kuishi maisha marefu,” alisema bibi huyo.
Comments
Post a Comment