Mbunge Kunambi akagua ujenzi wa madarasa anayotekeleza ujenzi wake Kata ya Mchombe


 


MBUNGE wa Jimbo la Mlimba Mkoani Morogoro, Godwin Kunambi amefanikisha azma yake ya kumaliza changamoto ya Maji katika Shule ya Sekondari Nakaguru iliyopo katika Kata ya Mchombe.

Kunambi amekamilisha ahadi ya kupeleka maji katika Shule hiyo yenye kidato cha kwanza hadi cha sita ikiwa ni matunda ya ziara yake aliyofanya Februari mwaka huu ambapo wanafunzi wa shule hiyo walimlalamikia changamoto hiyo.

Awali wanafunzi wa shule hiyo walikua wakisafiri umbali wa kilomita moja kufuata maji lakini sasa watachota maji ndani ya eneo la Shule hiyo.

Kunambi pia amefanikisha upatikanaji wa Bomba la maji mserereko kwa wananchi wa kijiji cha Nakaguru katika kata hiyo ya Mchombe.


Katika ziara hiyo pia Kunambi ametembelea Shule mbili moja ikiwa Shule ya Msingi Ngai ambayo amefanikisha kuanza kwa Ujenzi wa Darasa ambapo awali wanafunzi wa darasa la sita walimlalamikia kusoma kwenye darasa la wazi.

"Ni furaha yangu kuona nimekamilisha ahadi yangu kwa Sekondari ya Nakaguru ya kuwaletea Maji hapa lakini pia kufanikisha kuanza kwa Ujenzi wa Darasa hapa Ngai ambapo mwanzo walikua wakisoma kwenye darasa la wazi ambapo wanafunzi waliteseka nyakati za Mvua.


Ziara yangu hii pia nimekagua ujenzi wa madarasa mawili ya Shule ya Msingi Nakaguru ambayo yameshakamilika pamoja na madawati yake na sasa wanafunzi watasoma bila tabu,"Amesema Kunambi.

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Mchombe, Bathelomeo Swala amemshukuru Mbunge Kunambi kwa kufanikisha ahadi zake hizo ambapo amesema ujenzi wa madarasa hayo vitakua chache kwa wanafunzi hao kusoma kwa bidii.

Nae mmoja wa wanafunzi wa Sekondari ya Nakaguru Imelda John amemshukuru Mbunge Kunambi kwa kuwaletea maji kwani ilikua ni changamoto ya muda mrefu kwao hivyo sasa wana uhakika wa kupata maji safi kwenye Shule yao.

Comments