Waamuzi Masumbuko Matata wa Mwanza na Enock Akyoo wa Mtwara ambao walichezesha pambano la mwisho la Klabu bingwa ya Netiboli kati ya TAMISEMI QUEENS na JKT Mbweni ambalo lilimalizika kwa timu ya JKT Mbweni kushinda kwa magoli 40-39 wamelalamikiwa vikali na wadau wa mchezo huo kwa kuibeba timu mojawapo katika mchezo huo uliopigwa juzi katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha.
Katika pambano hilo kali na la kusisimua lililoshuhudiwa na mgeni rasmi Naibu Waziri, Wizara ya Habari Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Paulina Gekul wadau hao wameitaka CHANETA kuwachukulia hatua kali waamuzi hao kwa kuboronga kwa makusudi ili kuibeba timu ya JKT Mbweni.
Miongoni mwa walioshuhudia mchezo huo ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha Dkt Athumani Kihamia ambaye baada ya mchezo kumalizika alizungumza na waandishi wa habari na alionyesha dhahiri kukerwa na Kitendo cha Mwamuzi Matata kutoka Mwanza kushindwa kuumudu mchezo huo.
“Huyu refa aliyechezesha mchezo wa leo kutoka Mwanza mimi siwezi kumung’unya maneno hakuchezesha kihalali na tunaweza kusema ameyatia aibu mashindano haya,” amesema Dkt Kihamia.
Dkt Kihamia ambaye pia ni Mwenyekiti wa Michezo mkoa wa Arusha amesema anatarajia tukio kama hilo hataliona mwakani katika mashindano ya Ligi daraja la kwanza na badala yake aliwataka CHANETA kuhakikisha kuwa mashindano hayo yanaamuliwa na marefa walio huru na uwezo.
“Kwa refa kuchezesha vile ama hana uwezo au kachukua rushwa ama timu mojawapo inamhusu, kwa hiyo mwakani tutahakikisha mambo ya namna hii hayatokei katika mkoa wetu,” alisema Dkt Kihamia.
Kwa upande wake Mhe. Gekul wakati akiyafunga rasmi mashindano hayo aliwataka CHANETA kuhakikisha inateua waamuzi bora na wenye weledi wa kuchezesha mashindano ya ligi daraja la kwanza katika michezo kama hiyo mwakani.
“CHANETA hakikisheni waamuzi ambao mnawapa jukumu la kuchezesha michezo hii wawe ni waamuzi ambao hawafumbii macho jambo lolote linalofanyika uwanjani ambalo siyo la haki, ili atakayeshinda ashinde kwa haki na atakayeshindwa ashindwe kwa haki,” alisema Mhe.Gekul.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Klabu ya Michezo ya TAMISEMI Philbert Rwakilomba alieleza wazi kukerwa na kitendo cha waamuzi hao kuibeba timu ya JKT Mbweni katika mchezo huo kinashusha maendeleo ya mchezo huo kwani timu yake licha ya kuonyesha mchezo mzuri haikutendewa haki hasa na mwamuzi namba moja.
“tulitegemea kwa kuwa mchezo huu ndiyo uliokuwa ukiamua Klabu ipi kati ya hizo mbili kubeba ubingwa wa mchezo wa Netiboli mwaka huu, tushuhudie mchezo mzuri lakini kwa kweli nilichokiona hapa ni maamuzi ya marefarii wetu kuegemea upande wa wapinzani wetu,” alisema Rwakiloma
Kwa upande wake Nahodha wa TAMISEMI QUEENS Sophia komba alisema kuwa baada ya kuona waamuzi wameegemea upande mmoja alilazimika kupeleka malalamiko yake kwa mwamuzi wa akiba baada ya robo ya pili ya mchezo lakini hakuna hatua zozote zilizochukuliwa.
Miongoni mwa wananchi waliofurika kuutazama mchezo huo ni pamoja na Benson Maneno ambaye pia ni Afisa michezo wa Jiji la Arusha ambaye alisema kuwa waamuzi waamuzi hao waliipendelea JKT Mbweni huku Juma Athumani, mkazi wa Arusha yeye alisema kama siyo JKT Mbweni kucheza kibabe na Mwamuzi kuwabeba TAMISEMI QUEENS wangeifunga Mbweni JKT siyo chini ya magoli manane.
Katika mchezo huo wa mwisho wa klabu bingwa ligi daraja la kwanza timu ya Mbweni JKT ilishinda mchezo huo, huku TAMISEMI QUEENS ikishika nafasi ya pili.
Pia timu ya TAMISEMI QUEENS ilifanikiwa kutoa mfungaji bora wa mashindano hayo Lilian Jovin, Mchezaji bora wa mashindano hayo (MVP) Meryciana Kizenga na Mchezaji bora wa kati wa mashindano hayo Sophia Komba.
Jumla ya timu 13 zilishiriki mashindano hayo timu tisa za wanawake na timu nne za wanaume, ambapo washindi watatu wa kwanza wataiwakilisha nchi katika mashindano ya Netiboli Afrika Mashariki na timu sita za mwanzo zitashiriki katika kombe la Netiboli Zanzibar katika mashindano yatakayofanyika baadaye mwaka huu.
Comments
Post a Comment