Maonyesho ya mbegu na vyakula vya asili yafana Manyara


KATIBU Tawala wa Wilaya ya Babati, Mkoani Manyara, Khalfan Matipula, amezindua maonyesho ya mbegu na vyakula vya asili yaliyohusisha mikoa minne kwa kuitaka jamii kutumia vyakula vya asili vinavyoimarisha afya za walaji.

Matipula akizungumza mjini Babati kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa huo Charles Makongoro Nyerere amesema mbegu kuwa ghali husababisha wakulima kushindwa kumudu gharama au mbegu husika kushindwa kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.

“Mazao kama ngano, mpunga na mahindi ndiyo yanaliwa kwa wingi hivi sasa sehemu mbalimbali duniani na kumekuwa na msisitizo wa uzalishaji mazao hayo na uboreshaji wake,” amesema Matipula.

Meneja miradi wa shirika la PELUM Tanzania, Rehema Fidelis amesema maonyesho hayo yameshirikisha wakulima wa mikoa ya Manyara, Arusha, Kilimanjaro na Dodoma.

Fidelis amesema lengo la maonyesho hayo ni kupanua wigo wa wakulima na walaji kuchagua aina mbalimbali ya mbegu za asili ambazo nyingi hazizalishiwi tena.

Mkurugenzi wa shirika lisilo la kiserikali la Community Support Initiative Tanzania COSITA, Patrice Gwasima, amesema wakulima hao wamejifunza namna mbalimbali wenzao wanavyofanikiwa kupitia mikoa tofauti.

Gwasima amesema maonyesho hayo yameshirikisha viongozi wawakilishi wa ngazi mbalimbali, watafiti, wakulima na mashiriki yasiyo ya kiserikali.

Meneja miradi wa shirika la Islands of peace, Ayesiga Buberwa amesema maonyesho hayo yatawezesha uunganishaji na masoko na kuhamasisha uchakataji wa mazao ya kilimo na kuongeza thamani.

“Maonyesho ya mbegu za asili yataweka mazingira ya hali ya juu ya mwingiliano wa mahusiano kati ya walaji na wazalishaji,” amesema Buberwa. 

Mmoja kati ya wakulima walioshiriki maonyesho hayo, Fatuma Hondi amesema maonyesho hayo yatawajengea uwezo zaidi washiriki hao.

Hondi amesema kwa vile wamekutana wakulima wa maeneo mbalimbali watabadilishana ujuzi na namna ya kutatua changamoto zinazowakabili ili wapige hatua kubwa.

Mkulima wa Kata ya Kisimani wilayani Same mkoani Kilimanjaro, Haji Jumbe amesema wanatumia mbegu za asili za alizeti zenye miiba ili kuwazuia tembo wasiharibu mazao yao.

“Tunapakana na hifadhi ya Taifa ya Mkomazi hivyo ili kukinga mazao yetu yasiliwe na wanyamapori tunatumia mbegu za asili za alizeti yanye miiba na kutoa harufu ili kuwafukuza”  amesema Jumbe.

Comments