Baada ya kuwepo malalamiko kutoka kwa Wananchi wa Mikocheni Wilayani Kinondoni, Dar es Salaam juu ya uchafuzi wa mazingira unaosababishwa na moshi wa Viwandani, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Selemani Jafo amekitaka Kiwanda cha uchakataji Chuma Chakavu cha Iron & Steel Ltd kuhakikisha ifikapo Oktoba mwaka huu kero hiyo ya moshi wa viwandani inatatuliwa haraka.
Waziri Jafo ameyasema hayo alipofanya ziara katika Kiwanda hicho mapema leo Agosti 30, 2021 mkoani Dar es Salaam akiongozana na baadhi ya Maafisa wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazigira (NEMC).
Jafo ameagiza kutekelezwa kwa maagizo hayo awali yaliyowasilishwa na NEMC Kiwandani hapo kutokana na kilio cha Wananchi hao. “Mimi huwa sipendi mchezo, nimeambiwa wanakuja Maafisa wa Serikali mnawanunua na hakuna kitu kinachofanyika, Wananchi bado wanalalamika kuhusu moshi unaotoka Kiwandani kwenu, sitaki maneno nataka ifikapo mwezi Oktoba mwaka huu kero hii ya moshi iwe imetatuliwa haraka iwezekanavyo”, amesema Jafo.
Katika hatua nyingine, Jafo amesema alitaka kutoa maagizo ya kufunga Kiwanda hicho lakini kutokana na maslahi mapana ya Serikali ya Tanzania ameona haina haja ya kufunga kwa kuwa vijana wengi wa Kitanzania watakosa ajira na Serikali kukosa mapato yake kupitia Viwanda hivyo.
“Mwezi Novemba mwanzoni nakuja hapa kukagua maagizo haya niliyoyatoa leo, nikikuta hamjatatua kero hii inayosumbua Wananchi, basi sitoi Hati ya Uchakataji Chuma Chakavu hadi mrekebishe mazingira na yaridhishe Wananchi wote”, ameeleza Jafo.
Kwa upande wao Kiwanda cha Iron & Steel Ltd, kupitia kwa Afisa Rasilimali Watu, Idrissa Ali amesema wamesikia na kupokea maagizo hayo ya Waziri Suleiman Jafo na wameahidi kuyafanyia kazi ili ifikapo mwezi Oktoba wakamilishe na watatue kero hiyo ya moshi unaotoka Viwandani.
Comments
Post a Comment