Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imejipanga kufanya mpango wa matumizi bora ya ziwa Victoria ambao utaainisha maeneo ambayo yatatumika kufanya ufugaji wa vizimba ili kutoa nafasi pia kwa shughuli za uvuvi wa asili kuendelea bila kuwa na muingiliano.
Ulega aliyasema hayo Septemba 27, 2021 alipotembelea eneo la Kampuni ya Kichina ya Tangreen iliyowekeza katika mradi wa ufugaji wa Samaki kwa kutumika vizimba kandokando ya ziwa Victoria, jijini Mwanza.
Alisema kuwa serikali imedhamiria kufanya hivyo ili kupunguza muingiliano wa shughuli za ufugaji wa Samaki na Uvuvi wa asili ili shughuli zote zifanyike kwa ufanisi na kuleta tija katika uchumi wa buluu.
“Mpango wa Serikali ni kuhakikisha ufugaji wa vizimba unafanyika katika maeneo maalum na sio kila mahala, tuwe na maeneo mahsusi ya kazi hii ili kutoa nafasi pia wavuvi wa asili waweze kuendelea na shughuli zao,” alisema Ulega
Waziri Ulega alisema kuwa mpango huo pia utavutia wawekezaji wengi kuwekeza katika ziwa Victoria, na wao kama Serikali wanawakaribisha wawekezaji kama TanGreen kuja kuwekeza nchini.
“Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan imeweka mazingira mazuri ya uwekezaji, na hivi karibuni tumemuona akifanya jitihada kubwa kwa kuitangaza nchi yetu katika Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa, kufungua milango ya uwekezaji, na moja ya maeneo ya uwekezaji aliyokuwa akiyatangaza ni katika uchumi wa buluu,” alisema Ulega
Aliongeza kuwa TanGreen imejikita katika kukuza uchumi wa buluu kwa kufuga Samaki wa vizimba na wanatarajia kuvuna Tani Elfu kumi (10, 0000) kwa mwaka, huku akisema kuwa kwa sasa nchini samaki wanaovuliwa kutoka kwenye mabwawa ni Tani Elfu Ishirini na Mbili (22,000) hivyo TanGreen wanakwenda kuzalisha nusu ya kile kinachozalishwa sasa nchini.
Aidha, alimuelekeza Mkuu wa Wilaya ya Magu, Salim Mkali kuhakikisha muwekezaji huyo analindwa, na kama kutakuwa na wadokozi wenye nia ya kuirudisha nyuma kampuni hiyo wawachukulie hatua kali.
Ulega aliendelea kusema kuwa bado kunahitajio kubwa la Samaki nchini, kiasi kinachohitaji kwa mwaka ni Tani Laki Saba (700, 000) wakati uwezo uliopo kwa sasa Ni kuzalisha Tani Laki Nne (400, 000) hivyo kufanya pungufu ya Tani Laki Tatu (300,000) huku akisema ufugaji wa vizimba ukifanyika vizuri utasaidia kupunguza changamoto hiyo nchini.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Ruhumbi alisema kuwa wamejipanga kuufanya Mkoa huo kuwa mzalishaji mkubwa wa Samaki wa kufugwa katika mabwawa.
Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Rashid Tamatamah alisema kuwa Wizara kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wameendelea kuhamasisha uwekezaji wa mitaji na wamehamasisha mabenki kama Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) na imeshaanza kutoa mikopo, huku akisema wanaendelea kuwashawishi wawekeza wakubwa wa mitaji kuwekeza katika ufugaji wa samaki na kukuza uchumi wa buluu.
“Hivyo unaweza kuona kuwa ushawishi tulioufanya ndio umepelekea wawekezaji wakubwa kama TanGreen kujitokeza na kwa kweli imeleta tija kwa sababu miaka mitatu iliyopita kulikuwa na vizimba 18, lakini kwa sasa tunavizimba 473 na asilimia 77 ya vizimba vyote vipo hapa ziwa Victoria,” alisema Dkt. Tamatamah
Awali, Daktari wa Samaki wa Kampuni ya TanGreen, Dkt. Mugure Katwiga Mariwanda akisoma taarifa fupi ya Kiwanda hicho alisema kuwa moja ya lengo la Kampuni hiyo ni kukuza na kutangaza teknolojia ya ufugaji ikiwemo kufungua fursa ya ajira kwa vijana.
“Mhe. Naibu Waziri, pamoja na jitihada tunazoendelea nazo lakini tunakumbana na changamoto kadhaa ikiwemo uhaba wa vifaranga vya Samaki ndani ya nchi, baadhi ya wavuvi kuingia ndani ya mradi kuiba au kuharibu miundombinu,” alisema Dkt. Katwiga Mariwanda
Aliongeza kwa kuiomba Serikali itoe vibali vya kuingiza vifaranga vya samaki kutoka nje ya nchi ili kukidhi mahitaji yaliyopo huku akiiomba Serikali iendelee kutoa elimu kwa jamii ya wavuvi juu ya uwekezaji wa vizimba ili waache kufanya shughuli za uvuvi katika mradi huo.
Comments
Post a Comment