Kifo cha Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji, William Olenasha kimewagusa wengi lakini wabunge wamesema alikuwa kiongozi asiye na makuu.
Olenasha amefariki dunia jana Jumatatu Septemba 27, 2021 nyumbani kwake mtaa wa Medeli jijini Dodoma huku sababu za kifo chake zikiwa bado hazijawekwa wazi.
Kifo cha mbunge huyo wa Ngorongoro kinafikisha idadi ya wabunge waliofariki dunia tangu kuanza kwa Bunge la 12 kufikia watano. Wengine waliofariki dunia ni Martha Umbula, Khatib Said Haji, Atashasta Nditiye na Elias Kwandikwa.
Olenasha aliukwaa ubunge mwaka 2015 na aliteuliwa kuwa nabu waziri wa elimu na mwaka 2020 aliteuliwa kuwa naibu waziri wa mambo ya nje na baadaye alipelekwa ofisi ya waziri mkuu uwekezaji kuwa naibu waziri.
Wakizungumzia kifo cha Olenasha, mbunge wa Liwale Zuberi Kuchauka amemtaja kama mtu ambaye hakuwa na makuu katika nafasi alizopitia kwa miaka sita ya ubunge wake.
Kuchauka amesema kwa kwa miaka hiyo, hakuwahi kukwazana wala kumuona Olenasha akizungumziwa mabaya na mbunge yeyote hivyo wanaona wamepoteza mtu muhimu sana kwao ambaye mchango wake ulikuwa bado ukihitajika.
"Kama Kuna mtu anamzungumza vibaya yule mmasai (Olenasha) basi ana jambo lake, ukimfuata na jambo lako anakuambia subiri anapiga simu na kukupa majibu kwa hiyo hakukaa na viporo," amesema Kuchauka.
Mbunge wa Mpanda Vijijini, Seleman Kakoso amesema alikuwa mtaratibu ambaye hakuwa na papara hasa alipofuatwa na wabunge kutoa majibu.
Kakoso amesema atamkumbuka zaidi Naibu Waziri huyo katika kipindi Cha kwanza alipokuwa Naibu Waziri Wizara ya Elimu ambapo alisaidia mambo mengi jimboni kwake
Waziri wa Maji Jumaa Aweso amesema hawezi kumzungumzia Olenasha kwa leo kwa kuwa alikuwa akiendelea na vikao vingine.
Katika nyumba aliyokuwa akiishi eneo la Medeli maarufu maghorofa ya Serikali kulikuwa na watu wachache wakiendelea na maandalizi ya msiba.
Wakati huo Spika wa Bunge, Job Ndugai ametoa salamu za pole kwa Serikali na familia.
Comments
Post a Comment