Wananchi wa Madaba hatarini kukosa maji kutokana na kuharibiwa vyanzo vya maji



Na Amiri Kilagalila,Mahanje

Wananchi wa kijiji cha Mahanje kilichopo halmashauri ya wilaya ya Madaba mkoani Ruvuma wapo hatarini kuugua kutokana na maji wanayotumia kuwekwa dawa na baadhi ya wakulima wanaolima mazao katika vyanzo vya maji.

Aidha wananchi wa kijiji hicho pia wanaweza kukosa kabisa maji hapo mbeleni kutokana na kukauka maji hali inayosababishwa na Kilimo kinachoendelea karibu na vyanzo vya maji pamoja na ukataji wa miti hovyo.

Hayo waliyasema kijijini hapo na wananchi wakati wakizungumza na waandishi wa habari kuelezea kero hiyo ambayo imechukua muda mrefu pasipo kupata utatuzi.

Walisema kwenye kijiji hicho kuna vyanzo viwili tu vya maji ambavyo vimeharibiwa na baadhi ya wakulima  wanaofanya shughuli za binadamu katika milima na kupelekea uharibu wa vyanzo hivyo vya maji.

Walisema maji wanayokunywa kwasasa yana dawa ambazo wakati wa kunyunyiza kwenye mazao zimekuwa zikienda kwenye vyanzo vya maji ambayo wananchi hao wanayatumia.

Walisema licha ya juhudi za viongozi wa serikali katika kuzuia shughuli za binadamu katika vyanzo vya maji lakini wakulima hao wamekuwa wakikahidi maagizo hayo.

Walisema baadhi ya wafugaji kutoka kijiji cha Matetereka wamekuwa wakichunga katika maeneo ya vyanzo vya maji na kusababisha uchafuzi wa maji hayo.

Baadhi ya wananchi hao wakiwemo Vestina Ngatunga, Gerlod Mwenda  na Uric Kinyero walisema zaidi ya miaka mitatu wamekuwa wakifanya jitihada mbalimbali za kuondoa tatizo hilo lakini mpaka sasa muafaka haujapatikana.

Walisema kuendelea kwa shughuli za binadamu kwenye vyanzo hivyo vya maji ikiwemo ukataji wa miti unasababisha kupungua kwa kiwango cha maji kwenye vyanzo hivyo.

"Mwaka 2019 tulienda kwenye vyanzo vya maji tukakuta wakulima wanalima maharage na kutumia dawa ili kuulia zile nyasi tulichukua maji kwenye chupa na kuyaleta kwa viongozi wa kijiji ili kuona kama yanafaa kwa matumizi ya binadamu" alisema Uric.

Mwenyekiti wa watumia maji wa kijiji cha Mahanje Adelat Kilewa alisema tatizo hilo la wananchi kunywa maji machafu ni la muda mrefu tangu hajaingia madarakani lakini utekelezaji wake umekuwa hafifu kwenye kutatua tatizo hilo.

Alisema viongozi wa serikali wamekuwa wavivu katika kutatua matatizo ambayo wananchi yanawakabili.

Alisema wakati wa ziara ya mbunge wa jimbo hilo la Madaba Joseph Mhagama  wananchi walitoa kero hiyo huku wakimuonyesha maji kwenye kopo ambayo hayastahili kwa matumizi ya binadamu.

"Maji yanapatikana kwa kusuasua na machafu zaidi Hawa wenzetu wa milimani wanapiga dawa na najua baada ya muda wananchi hawa ambao ni watumia maji watapata kansa" alisema Kilewa.

Mtendaji wa kijiji cha Mahanje Jabir Fuse alikiri kuwepo kwa changamoto hiyo ya kuchafuliwa kwa vyanzo vya maji ambapo hatua alizochukua Ni kuwakamata wananchi wa kijiji hicho waliokuwa wanafanya shughuli za binadamu katika vyanzo vya maji.

Alisema shida kubwa inayofanya vyanzo hivyo vya maji kuchafuka ni wakulima ambao wamekuwa wakilima vinyungu na kusababisha kuchafuka kwa maji hayo.

"Changamoto iliyopo katika vyanzo hivyo vya maji kuna sehemu ya mipaka katika kijiji cha Mahanje na Matetereka  ambacho hakipo katika eneo la utawala wangu" alisema Fuse.

 

Comments