Jaji mkuu aanza ziara ya kikazi katika Mahakama ya Tanzania, Kanda ya Musoma



Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma ameanza ziara ya kikazi ya siku nne katika Mahakama ya Tanzania, Kanda ya Musoma, kukagua shughuli mbalimbali za kimahakama, ujenzi wa miundombinu pamoja na kuongea na watumishi wa kada zote.

Katika siku yake ya kwanza ya ziara, Mhe. Jaji Mkuu ametembelea Mahakama ya Mwanzo Kukirango iliyopo katika eneo la Kiabakari Wilaya ya Butiama, Mkoa wa Mara na kupokea taarifa ya utendaji katika Mahakama hiyo kutoka kwa Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mhe. Kulwa Sanya.

Katika taarifa yake, Mhe. Sanya alimweleza Prof. Juma kuwa Mahakama yake hupokea mashauri kutoka katika kata saba za wilaya ya Butiama ambazo ni Butiama, Kukirango, Buruma, Nyankanga, Kyanyari, Bukabwa pamoja na Masaba. 

Akielezea hali ya usikilizaji wa mashauri katika Mahakama hiyo, Hakimu Mfawidhi alieleza kuwa ili kutekeleza dira ya Mahakama ya Tanzania, watumishi wa Mahakama ya Mwanzo Kukirango wamefanikiwa kumaliza wastani wa asilimia 113.86 ya mashauri yote yaliyopokelewa kuanzia mwezi Januari hadi September 2021.

“Tumefanikiwa kufanya hivyo baada ya kufanyia kazi maelekezo yanayotolewa mara kwa mara na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Musoma; Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Musoma; pamoja na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Musoma katika vikao na semina za ndani,” amesema. 

Akifafanua hatua hiyo, Mhe. Sanya alimweleza Jaji Mkuu kuwa mashauri yaliyobaki Disemba 2020 yalikuwa 64 na katika kipindi cha mwezi Januari hadi Septemba 2021, mashauri yaliyofunguliwa yalikuwa 303, yaliyoamliwa katika kipindi hicho yalikuwa 345 na mashauri ambayo yamebaki hadi Septemba ni 22 tu.

Baada ya kupokea taarifa hiyo, Prof. Juma alitembelea ujenzi wa Mahakama ya Wilaya ya Butiama ambapo Mhandisi Bakari Seif alitoa maelezo mafupi juu ya mradi huo unaotekelezwa na kampuni ya ‘Builders Limited’ unatarajiwa kukamilika kwa kipindi cha miezi sita.

Awali, Jaji Mkuu alipata nafasi ya kusalimiana na Mkuu wa Wilaya ya Butiama, Mhe. Moses Kaegele, ambaye aliushukuru uongozi wa Mahakama ya Tanzania kwa uamuzi wa kujenga Mahakama hiyo ya wilaya ambayo itakuwa na manufaa makubwa kwa wananchi wa wilaya yake.

Amesema kuwa wananchi walikuwa wakisafiri umbali mrefu kwenda Musoma mjini kutafuta huduma za kimahakama, hivyo ujenzi wa mahakama hiyo utawapunguzia muda wa kupata huduma hizo na hivyo kushiriki katika shughuli zingine za kujipatia kipato.

Baadaye Jaji Mkuu alielekea Wilaya ya Bunda ambapo alifanya mazungumzo na Mkuu wa Wilaya hiyo, Mhe. Joshua Nasari, ambaye akiwa kama Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya Wilaya, alimhakikishia ushirikiano katika nyanja zote ili Mahakama ya Tanzania iweze kutimiza jukumu lake ipasavyo la utoaji haki kwa wananchi.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Musoma, Mhe. John Kahyoza alimshukuru Mkuu wa Wilaya kwa ushirikiano aliouonesha hasa wa hivi karibuni ambao ulichangia kuokoa takribani millioni 26 katika kukamilisha ujenzi wa Mahakama hiyo.

Prof. Juma pia alipata nafasi ya kukagua jengo jipya la Mahakama ya Wilaya ya Bunda na pia kuongea na watumishi wa Mahakama hiyo baada ya kupoke taarifa ya utendaji iliyotolewa na Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mhe. Mulokozi Kamuntu.

Katika taarifa yake, Mhe. Kamuntu alimweleza Prof. Juma kuwa katika kipindi Januari hadi Oktoba, 2021 jumla ya mashauri 406 yalisajiliwa kwenye mfumo na mengine 391 yaliyoisha yameondolewa kwenye mfumo huo na kufanya mashauri yaliyopo mpaka sasa kuwa 227.

Alisema kuwa idadi ya mashauri yaliyobaki hadi Disemba 2020 yalikuwa 212, mashauri yaliyofunguliwa Januari hadi tarehe 25 Oktoba, 2021 yalikuwa 406, yale yaliyoamuliwa kwa kipindi hicho yalikuwa 391 na ambayo yamebaki yapo 227.

Katika ziara hiyo, Jaji Mkuu atatembelea maeneo mbaloimbali, ikiwemo Wilaya ya Serengeti, Tarime na Rorya.

Comments