Kilosa kutumia bilioni 4 za IFM kuimarisha afya na elimu



WILAYA ya Kilosa mkoani Morogoro imepata mgao wa Sh bilioni 4.33 kutoka kwenye fedha zilitolewa na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), kwa Serikali ya Tanzania.

Mgao huo wa Sh bilioni 4.33 uliopelekwa Kilosa na Serikali ni kati ya Sh, trilioni 1.3 ambayo imetangazwa na Rais Samia Suluhu Hassan hivi karibuni kuwa zitatumika kwenye kutekeleza miradi mbalimbali kwenye sekta ya afya, elimu, maji, viwanda na nyingine.

Akizungumza na mwandishi wa habari hii Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Alhaj Majid Mwanga amesema fedha hizo zitatumika kutekeleza miradi mipya kupitia mpango wa maendeleo  kwa usatawi wa taifa na mapambano dhidi ya Uviko-19 ambapo wilaya hiyo imepata fedha kwenye sekta ya elimu na afya.

Alhaj Mwanga amesema Sh bilioni 2.94 zitatumika kujenga vyumba 147 vya madarasa ya shule za sekondari na Sh milioni 780 zitajenga vyumba vya madarasa 39 ya vituo shikizi 13.

“Shilingi milioni 420 zitatunua mashine za mionzi katika Hospitali ya Mikumi, Sh milioni 100 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya wagonjwa mahututi na Sh milioni 90 zitajenga nyumba za watumishi,” alisema.

Mkuu huyo amesema wamejipanga kusimamia vizuri mchakato mzima wa ujenzi wa miradi hiyo na kutoa angalizo kwa watu ambao wanatarajia kutumia miradi hiyo kwa manufaa binafsi.

Mwanga amewataka watendaji wote kuanzia ngazi ya kitongoji hadi wilayani ambao wanahusika na utekelezaji wa miradi hiyo kujituma ili miradi ikamilike kwa wakati.

“Kwa niaba ya wananchi na viongozi wa Kilosa, napenda kumshukuru Rais Samia na Serikali yake kutupatia kiasi hiki cha fedha ambacho kinaenda kufanya mapinduzi katika sekta husika. Ninapenda kumhakikishia kuwa tupo pamoja na yeye na hatutavumilia mtu yoyote ambaye atajaribu kuenda kinyume na malengo,” alisema.

Alhaj Mwanga amesema iwapo kila mmoja atatimiza malengo yake kwa weledi ni wazi kuwa Kilosa itabadilika na kupata maendeleo kwa haraka.

Comments