MKOA wa Manyara imeelezwa kuwa una kiwango cha juu cha ukeketaji kwa wanawake wa eneo hilo kuliko mikoa mingine nchini kwa asilimia 70.8.
Mratibu wa mtandao wa kuelimisha jamii juu ya madhara ya ukeketaji na aina nyingine za unyanyasaji wa kijinsia (NAFGEN) Francis Selasini amesema kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Tanzania Demographic Survey, Manyara inaongoza kwa ukeketaji.
Selasini amesema mikoa inayofuata ni Dodoma asilimia 63.8, Arusha asilimia 58.6, Singida asilimia 51, Mara asilimia 39.9, Kilimanjaro asilimia 21.7 na Morogoro asilimia 21.1.
Amesema utafiti wao wa kiutendaji una wahakikishia kuwa ukeketaji upo vijijini kwa asilimia 100 na hivi sasa wanakeketa watoto wakiwa wadogo ili kukwepa mkono wa sheria.
Amesema ukeketaji unaendana na ndoa za utotoni kwani kuna tofauti kubwa kati ya thamani ya mwanaume na mwanamke kielimu katika maeneo hayo.
"Katika jamii za mkoa wa Manyara inaona kuwa kuliko mtoto wa kike apate mimba akiwa nyumbani na kuwapa aibu ni bora akaolewe katika umri mdogo" amesema Selasini.
Anasema hivi sasa wanachanganya sherehe za wavulana na wasichana ili wasijulikane kwa urahisi japo elimu inawafikia na wanaelewa ila kubadili fikra ndiyo tatizo.
Ofisa maendeleo ya jamii wa mkoa wa Manyara, Anna Fissoo anasema ukeketaji unafanywa kwa asili ikiwa ni mila na desturi kwani mwanamke asipofanyiwa hivyo hakubaliki kwenye jamii.
Fissoo anasema Serikali ya eneo hilo ilipoingilia kati suala hilo jamii ilibadilisha aina waliyokuwa wanatumia kwa kuwapeleka watoto kwa bibi zao vijijini ili wakakeketwe huko.
Amesema jamii za wilaya za Kiteto, Hanang' na Simanjiro, ndiyo zimekithiri kwa kuwa na matukio ya ukeketaji.
Mkazi wa kata ya Katesh, Paul Bura amesema jamii za wairaq, wadatoga, wamasai na wanyaturu ndiyo wamekithiri kwa kuwafanyia watoto wao matukio ya ukeketaji.
Bura anasema asasi za kiraia na viongozi wa serikali kupitia maofisa wa maendeleo ya jamii wamekuwa wakitoa elimu kwa jamii ili kuondokana na ukeketaji.
Mganga wa kituo cha afya Katesh, Dkt David Laizer anasema chanzo cha ukeketaji ni kuendeleza mila na desturi kupitia mfumo dume.
"Elimu ianze kwa wanaume kwani wanawake wanatambua madhara ya ukeketaji ila amri hutoka kwa wanaume na hawapingi" amesema Dkt Laizer.
Amesema miongoni mwa athari za ukeketaji ni kuvuja damu nyingi wakati wa kufanyiwa tukio hilo na kutoka damu nyingi wakati wa kujifungua.
Ametaja athari nyingine ni uwezekano wa mwanamke kupata fistula na wakati wa kujifungua anaweza kupoteza maisha.
Comments
Post a Comment