Waziri Mhagama akemea utoro wa dawa kwa WAVIU


WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama amekea vitendo vya baadhi ya watu wanaoishi na Virusi vya UKIMWI nchini kukwepa na kusitisha matumizi ya dawa za kupunguza makali ya ugongwa huo huku wakipatwa na madhara zaidi.

Ametoa kauli hiyo alipotembelea na kukagua shughuli za watu wanaoishi na Virusi vya UKIMWI kutoka katika Konga Jiji Mbeya, kukagua ujenzi wa Kituo cha Tiba na Matunzo (CTC) Chimala pamoja na ujenzi wa Kituo cha Tiba na Matunzo cha Zahanati ya Igawa Mbarali oktoba 27, 2021 Jijini Mbeya.

Waziri alieleza kuwa, kumekuwa na kesi za watu kutoroka na kusitisha matumizi ya dawa hizo huku akieleza kuwa ni changamoto inayokwamisha mapambana dhidi ya ugonjwa wa UKIMWI.

“Wanaoishi na VVU wote acheni kutoroka dawa bali endeleeni kutumia dawa hizo ili kuendelea kufubaza makali na kuwa afya njema,”alisema waziri Mhagama


Alisema ni wakati sasa jamii kuwa na uelewa wa kutosha kuhusu umuhimu wa dawa hizo kwani zimeendelea kusaidia watu wanaoishi na Virusi vya UKIMWI huku wakiimarika na kuendelea na shughuli zao za uzalishaji bila kuathiriwa na jambo lolote.

Aidha aliwakumbusha kuendelea kulindana wao kwa wao na kukumbushana matumizi sahihi ya dawa za kufubaza na kupunguza makali ya ugonjwa huo huku akiwasii kuendelea kujiandikisha na BIMA ya Afya ili kusaidia kupata huduma za afya.

“Hakikisheni kila mmoja anakuwa mlinzi wa mwenzake kwa kusisitiza matumizi sahihi ya dawa bila kukwepa na endeleeni kuhakikisha kila anayeishi na VVU anakuwa na Bima ya afya kwani itarahisisha kupata huduma za afya, mkakati huu ni mzuri napongeza sana,”alisema

Aidha alitumia fursa hivyo kuendelea kuwasihi wanaume kujitokeza kwa wingi kupima afya zao kwani imeonekana ni kundi ambalo lipo nyuma katika kujitokeza kujua hali zao.

Aidha aliagiza Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya kuendelea kuunga mkono mapambano hayo huku akimtaka kutoa kipaumbele kwa WAVIU katika utoaji wa mikopo isiyo na riba ili kuwakwamua na changamoto za mitaji

“Halmashauri endeleni kuchangia jitihada za watu wanaoishi na VVU na hakikisheni mnakuwa na kanzi data itayosaidia kuwafahamu na kuwafikia kwa wakati hii itasaidia katika shughuli za kujikwamua kiuchumi na kujiletea maendeleo yao,”alieleza waziri.


Akitoa taarifa ya hali ya masuala ya UKIMWI, Mwenyekiti wa Baraza la Watu wanaoishi na Virusi vya UKIMWI Mbeya, Bw. Douglas Kisunga alisema Halmashauri ina jumla ya konga kata 32 na vikundi wezeshi 54 vya shughuli za mwitikio wa masuala ya UKIMWI na kuhamasisha upimaji na kuwaunganisha WAVIU kutambuana na kusaidiana katika kujikwamua kiuchumi na kujiletea maendeleo yao.

Aliishukuru Serikali kuendelea kuwatambua na kuwaunga mkono katika shughuli zao za kila siku huku akieleza mafanikio ya konga hiyo, kwa kushirikiana na Halmashauri ya Jiji wamefanikiwa kuwa na umoja wa watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI, na kupata huduma za tiba na matunzo na kuhamasisha watu kujitokeza zaidi.

“Mwanzo WAVIU waliojitokeza kwa uchache ambapo walikuwa 53 tu, hadi sasa wamejitokeza na kufikia 1129 na wapo huru, wanaishi kwa raha na wanafuata maelekezo ya Serikali huku wakifurahia maisha,”alisema Kisunga

Aidha alieleza kwa kipindi cha Juni hadi Julai konga imefanikiwa kurudisha watoro wa dawa 132 ambapo wanaume ni 58 na wanawake 74 na kuhakikisha wanabaki katika huduma za tiba na matunzo.

Alifafanua kuwa, Konga zimefanikiwa kuwa mstari wa mbela katika mapambano dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto, kuendelea kuhamasisha upimaji wa hiari na matumizi ya dawa kwa kujilinda na kulinda wengine na kumekuwa na uwazi wa watu kujitokeza kueleza hali zao.

“Katika kujitokeza kupima na kujua hali wanaume wamekuwa na mwitikio mdogo ambapo kwetu waliojitokeza ni 622 wanaume na wanawake 1407 hivyo kundi la wanaume bado lipo chini tuendelee kuwahamasisha kujitokeza kujua hali zao ili wakikutwa na maambukizi wajiunge katika huduma za tiba na matunzo,”alisema

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti UKIMWI nchini Dkt. Leonard Maboko alitoa rai kwa kila mtanzania kutambua kuwa ugonjwa huu upo, watu wajitokeze kupima na kujua hali zao ili kuendeleza mapambano hayo na kupunguza hali ya maambukizi mapya nchini.

 

Comments