Dar Wapewa Siku Tisa Fedha Ziombwe Ujenzi Soko Kariakoo



WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tamisemi Ummy Mwalimu ametoa siku tisa kwa uongozi wa Mkoa wa Dar es Saalam kuandika barua ya kuomba fedha Hazina kwa ajili ya ukarabati na ujenzi wa soko jipya Kariakoo.


Ummy alitoa kauli hiyo Dar es Salaam jana wakati yeye pamoja na Naibu Waziri Fedha na Mipango, Hamad  Masauni walipolitembelea soko la Kariakoo na kuangalia maandalizi ya ukarabati wa soko la zamani lililoungua pamoja na ujenzi wa soko jipya.


Hatua ya Ummy imefuatia kauli ya Masauni kuwa fedha kiasi cha Sh bilioni 32.2 zilizotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya kufanikisha ujenzi huo zimeshatolewa na kilichobaki sasa ni utaratibu wa wahusika kwenda kuzichukua.


“Naelekeza fedha zilizotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan ziombwe na Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam sababu mradi huu ni mkubwa na wilaya watabaki kuwa wafuatiliaji wa karibu lakini Mkoa lazima wasimamie kikamilifu," alisema Ummy


Alisema sababu kubwa iliyomfanya kulitembelea soko hilo ni kufuatilia utekelezaji wa agizo la Rais Samia aliyetaka ukarabati wa soko hilo pamoja na ujenzi wa soko jipya litakalokuwa na uwezo wa kuwachukua wafanyabiashara zaidi ya 2,000.


Ummy alisema soko jipya la ghorofa sita juu na mbili chini, litakalojengwa katika eneo la soko dogo, kwa kiasi kikubwa litasaidia kuwapunguza wafanyabiashara waliopo katika eneo hilo la Kariakoo na hivyo kupunguza idadi ya wafanyabiashara wengi waliopo mitaani.


“Ninachotaka kuona ni soko linajengwa kwanza baadaye ndiyo tutajua namna ya Menejimenti kama lisimamiwe na Jiji au Shirika la Masoko Kariakoo, hapa lengo ni kuangalia kazi hii inakamilika mapema ili wafanyabiashara waweze kuingia na kuanza biashara haraka iwezekanavyo.


"Tunamshukuru Rais amesisitiza suala la kupangwa kwa mji kwa ajili ya kuifanya kuwa na usalama, changamoto hazikosekani hivyo ni vyema tuzitatue na kuupongeza Mkoa wa Dar es Salaam kwa jitihada kubwa wanazozichukua kuwapanga wamachinga,” alisema Ummy


Katika hatua nyingine  Ummy alisema malengo yake fedha hizo zitakapochukuliwa ufanywe utaratibu wa haraka utakaohakikisha ujenzi unaanza mara moja.


Kwa upande wake Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Hamad  Masauni  alisema tayari Wizara hiyo imekamilisha mchakato wa kupatikana fedha hizo na kuongeza kuwa kinachosubiriwa sasa ni utaratibu wa kuchukuliwa zikaanze kazi iliyokusudiwa.


Kwa mujibu wa Masauni, kiasi cha Sh bilioni sita kimetengwa kwa ajili ya ukarabati wa soko lililoungua huku kiasi cha Sh bilioni 26 zikitegwa kwa ajili ya ujenzi wa soko jipya

Comments