Kauli ya Rais Samia yaibua mjadala




Wakati Rais Samia Suluhu Hassan akiwataka viongozi wa siasa kumuenzi aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Hayati Maalim Seif Sharif Hamad kwa siasa za majadiliano, baadhi ya wanasiasa wamemtaka kutimiza kwanza ahadi yake ya kukutana na vyama vya siasa.


Rais Samia alitoa kauli hiyo juzi mjini Unguja, alipoizindua Taasisi ya Maalim Seif akisema kiongozi huyo alikuwa mtu aliyesimamia mambo anayoyaamini na kusimamia masilahi ya Taifa.


Maalim Seif alifariki Februari 17 mwaka huu, katika Hospitali ya Taifa Muhimbili alikokuwa akitibiwa na kuzikwa kisiwani Pemba Februari 18.


“Kama liko jambo linalompambanua Hayati Maalim Seif kwa usahihi kabisa, basi ni uthabiti wa misimamo yake na utayari wake wa kutafuta maridhiano pale inapotokea kusigana na kutofautiana katika jambo analoliamini.


“Hii si sifa ya kawaida kwa wanasiasa na viongozi wengi duniani, mtakubaliana nami kwamba mara nyingi katika nchi zetu zinazoendelea, wanasiasa wanapotofautiana kinachofuata ni vurugu isiyoisha,” alisema Rais Samia.


Rais pia alisema Maalim Seif tangu akiwa kiongozi na kada wa CCM alikuwa mtu mwenye misimamo yake aliyoisimamia na alijipambanua nayo.


“Tena wakati huo tukiwa katika mfumo wa chama kimoja, lakini bado alikuwa akisimama kwenye misimamo yake. Alipingana kwa hoja bila kumtusi au kumdhihaki mtu, wala kugombana na mtu, hakuogopa gharama ya kusimamia alichokiamini.


“Maalim Seif aliendelea kuwa yuleyule hata alipohamia upinzani na kuasisi Chama cha Wananchi (CUF) baada ya kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa nchini,” alisema Samia.


Akifafanua zaidi, Rais alisema Hayati Maalim Seif alikuwa chachu ya maridhiano yaliyosababisha kutokea mwafaka na hatimaye kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) visiwani humo.


“Pale ambapo tofauti zetu zilivuka mpaka na kusababisha kuvunjika kwa amani, Hayati Maalim Seif hakuacha kuonyesha utayari wa kuzungumza,” alisema.


Tabia yake ya kuzungumza kila kulipokuwa na tatizo, Rais alisema iliwezesha kupatikana kwa mwafaka wa kwanza baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2000 kati ya CCM na CUF waliolalamikiana kuhusu matokeo yaliyotangazwa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC).


“Hata pale mwafaka wa kwanza ulipolegalega, Hayati Maalim Seif hakukata tamaa, kwani tuliingia kwenye mazungumzo ambayo yalizaa mwafaka wa pili, hatimaye maridhiano ya mwaka 2010 ambayo yalijumuishwa katika Katiba ya Zanzibar ya 1984 toleo la 2010,” alisema.


Alimpongeza Rais mstaafu wa Zanzibar, Amani Abeid Karume kwa kushirikiana na marehemu Maalim Seif kufikia makubaliano yaliyounda Serikali ya Umoja wa kitaifa.


“Ni Hayati Maalim Seif tena aliyeshiriki na kuyafanikisha maridhiano baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020. Utayari wake wa kuangalia masilahi mapana ya Taifa umechangia vyama vya CCM na ACT-Wazalendo kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar na yeye kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais,” alisema Rais.


Wapinzani wahoji

Hata hivyo, baadhi ya wanasiasa waliozungumzia kauli hiyo ya Rais Samia wamemtaka kuyatekeleza maneno hayo kwa kurejea ahadi yake ya kukutana na vyama vya siasa aliyoitoa bungeni Aprili 22 mwaka huu.


“Rais alipozungumza bungeni alisema atakutana na wanasiasa wenzake kuzungumzia mwafaka wa kitaifa. Alikuwa amekaa madarakani mwezi mmoja, lakini mpaka leo kauli yake hajaitekeleza,” alisema James Mbatia, ambaye ni mwenyekiti wa Chama cha NCCR Mageuzi aliyekuwapo kwenye uzinduzi huo.


Hakuishia hapo, bali aliongeza kwamba “kauli yake siku anaapishwa Machi 19 ya kuleta umoja na tukae pamoja, hajaitekeleza. Sisi NCCR-Mageuzi tulimwandikia barua Mei 4 kumkumbusha kauli yake siku alipoapishwa, kauli aliyoitoa bungeni na kumwomba mwongozo kuhusu madhila yaliyotokana na uchaguzi.


“Ikulu wakatujibu Mei 18 wakisema Rais amepokea na atakutana nasi haraka iwezekanavyo. Mpaka leo hajatekeleza. Kusema ni jambo moja na kutekeleza ni jambo jingine. Kauli anazotoa ni maneno tu hakuna matendo.”


Kauli ya Mbatia imeungwa mkono na Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu anayeishi nchini Ubelgiji akitaka kauli za Rais zitekelezwe kwa vitendo.


“Aliahidi hadharani akiwa bungeni kukutana na vyama vya upinzani. Hadi sasa hajafanya hivyo. Aliahidi maridhiano na anazungumza majadiliano, lakini amekataza majadiliano kuhusu Katiba mpya na mikutano halali ya kisiasa. Anazungumza amani lakini anaendeleza vita dhidi ya demokrasia kama ilivyokuwa kwa mtangulizi wake,” alisema Lissu alipohojiwa kupitia mtandao wa WhatsApp.


Naye Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Zanzibar) Salum Mwalimu alisema: “Maalim Seif kwa kiwango kikubwa sana amechangia huu utulivu tulionao hivi sasa, angeweza kuwaambia watu waingie barabarani kudai haki zao, lakini hakufanya hivyo kwa kuwa alikuwa muumini wa umoja na maridhiano.”


Kwa upande wake Kiongozi wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe alisema chama hicho kitatekeleza mambo aliyoacha Maalim Seif ili kuenzi fikra zake na kuandaa viongozi wanaoweza kusimamia mawazo yao bila kujali wengine wana tafsiri zipi.


“Maalim alikuwa kinara wa siasa za utaifa, alikuwa tayari kugombana na yeyote anayejali masilahi ya chama au kundi fulani la watu, utajiri wake wa mawazo na busara tutaendelea kuukumbuka na kuuenzi, ACT-Wazalendo tunawahakikishia Watanzania kudumisha umoja, mshikamano na utulivu.


Mbali na wanasiasa, Mwanasheria maarufu visiwani Zanzibar, Awadh Said alisema angalau Rais Samia ameonyesha dhamira ya kutaka kukutana na vyama vya siasa, lakini suala la utekelezaji ndiyo halijulikani undani wake.


“Kwanza ameonyesha utayari na ameweka hadharani kwamba anataka kukutana na wanasiasa, nadhani sasa ni wakati mwafaka wa kujua kwa nini hatekelezi.


“Kuna msemo wa walk the talk (tekeleza unachosema), ni muhimu, lakini siwezi kujua undani wake ni upi na kwa wapinzani ni upi,” alisema Awadhi.


Kwa upande mwingine akimjadili Maalim Seif, mwanazuoni nguli wa sheria nchini, Profesa Issa Shivji alisema Maalim hakuandaa viongozi wengine wachukue nafasi zao wakati bado wako hai.


Alisema hata baada ya uchaguzi wa 2020, Maalim Seif alikuwa akisitasita kuingia katika SUK na alitaka aende mtu mwingine, lakini watu hawakutaka ndiyo maana alirudi yeye mwenyewe.


Akizungumza awali, Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi alisema Maalim Seif alikuwa mwanamaridhiano wa kweli huku kielelezo halisi kikiwa ni juhudi zake za kuhakikisha kuwa nchi inakuwa na amani na utulivu baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.


“Hayati Maalim Seif hakuwa mtu wa kujikweza, kiburi au majivuno, bali alikuwa aliweka maslahi ya Zanzibar kwanza, hakuwa mbinafsi wala mchoyo katika kushauri na kutoa hekima na nasaha zake kwa viongozi vijana kama sisi,” alisema Dk Mwinyi.


Mwenyekiti wa ADC, Hamad Rashid Mohamed alisema Maalim Seif Sharif Hamad alikwenda kutafuta mwafaka ya Zanzibar mwaka 2019 bila kukishirikisha Chama cha CUF hali iliyoleta mtikisiko.


“Nakumbuka Maalim aliniambia twende kwa wananchi, acha wakituzomea au wakifanya lolote lakini mimi najua tunachokifanya kitakuwa na faida kubwa kwa Taifa letu,” alisema Hamad.


Alisema baada ya Maalim kumaliza kikao kile kila mmoja wetu alishangaa watu walivyomuelewa na kumuamini, hivyo tukaanza kwenda kueleza faida ya maridhiano, Maalim alionekana ndiye kinara.

Comments