Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa amekemea tabia ya baadhi ya viongozi kudharau taratibu za kiusalama zilizowekwa kwenye viwanja vya ndege, ikiwamo ya ukaguzi na kukaguliwa.
Amesema viongozi hao ni pamoja na wale wanaofanya kazi katika viwanja hivyo vya ndege, waingiapo na watokapo.
Profesa Mbarawa aliyasema hayo alipokuwa akizindua Siku ya utamaduni wa usalama wa usafiri wa anga, iliyoandaliwa na Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) kwa kushirikiana na wadau, iliyofanyika Jijini Dar es Salaam.
Profesa Mbarawa alisema kila mmoja anayekuwa katika viwanja vya ndege analo jukumu la kusimamia usalama wa anga katika eneo husika.
Alisisitiza kuwa viongozi wana wajibu wa kusimamia sheria na kanuni zilizowekwa ili kuimarisha usalama.
Alisema anazo taarifa za watumishi, wakiwamo baadhi ya wakuu katika taasisi zinazofanya kazi katika viwanja vya ndege, hukaidi utekelezaji wa matakwa ya usalama kwa kudharau taratibu za ukaguzi zilizowekwa.
“Hili jambo si sahihi, mimi waziri mwenye dhamana ya sekta hii, nikipita mule (uwanja wa ndege) nahakikisha nakaguliwa, navua viatu na mkanda. Nafanya kila ninachotakiwa kwa mujibu wa sheria.
“Sasa nawashangaa kabisa… wakuu wa taasisi wa kiwanja hiki cha ndege wanataka nisikaguliwe. Hii siyo sahihi, naomba muelewe usalama wa viwanja hivi upo ndani ya mikono yetu, tukitekeleza wajibu wetu vitakuwa salama zaidi,” alisema Profesa Mbarawa.
Kutokana na umuhimu wa utamaduni wa usalama wa usafiri wa anga, Profesa Mbarawa aliziagiza taasisi zote zinazotoa huduma katika sekta hiyo kuwa na mikakati endelevu itakayoboresha usalama wa usafiri wa anga kwa viwanja vyote nchini.
Alisema miongoni mwa taasisi hizo ni TCAA, mashirika ya ndege, waendeshaji wa viwanja vya ndege, mawakala wa huduma za ndege pamoja na watoa huduma za vyakula kwenye ndege.
Awali, Mkurugenzi Mkuu wa TCAA, Hamza Johari alisema uzinduzi wa utamaduni wa usalama wa usafiri wa anga umebebwa na kauli mbiu ya ‘usalama wa usafiri wa anga ni jukumu letu sote’.
“Tukio la leo lina maana kubwa kimataifa, kwa sababu usalama ni kipaumbele cha kwanza katika sekta hii. Kukiwa na usalama kunasaidia kuongeza watumiaji wengi wa sekta ya anga,” alisema Johari.
Johari alisema tukio hilo limetokana na azimio la Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga (ICAO), linalotaka wadau kuhakikisha wanajijengea utamaduni wa kutambua usalama ni jukumu la kila mtu anayetumia usafiri wa anga kwenda popote atakapo.
Comments
Post a Comment