Wananchi Moshi walalamikia ongezeko bei ya nyama


 


Walaji wa nyama ya ng’ombe katika Manispaa ya Moshi, Mkoani Kilimanjaro wamelalamikia bei ya nyama hiyo kupanda ghalfa kutoka Sh8,000 na kufikia Sh10,000.


Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi leo Novemba 5 katika masoko ya mjini wa Moshi na kushuhudia baadhi ya maeneo nyama hiyo ikiuzwa Sh9,000 huku maeneo mengine nyama hiyo ikiuzwa kwa Sh10,000.


Wakizungumza na Mwananchi, baadhi ya wakazi wa mji wa Moshi wameiomba Serikali kuingilia kati mfumuko huo wa bei ya nyama kwani ongezeko hilo linakandamiza wananchi wenye kipato cha chini.


Annastela Urio mkazi wa Majengo amesema kupanda kwa bei hiyo ni kuwafanya watu wa hali ya chini kushindwa kumudu gharama ya kununua nyama hiyo kutokana na bei hiyo ambapo ameiomba serikali kuangalia namna ya kudhibiti upandaji wa nyama kiholela.


“Haya maisha yanakuwa magumu sasa juzi tuu nimenunua nyama Sh8000, leo nimekwenda kununua naambiwa imepanda bei hadi Sh9,000 na nasikia kuna maeneo mengine imepanda hadi Sh10,000. Sasa watu wenye kipato cha chini tutakimbilia wapi?” amesema Annastela. 


Mwananchi mwingine, Naye Asha Hussein ambaye ni mkazi wa mtaa wa Msaranga amesema kupanda kwa nyama hiyo kiholela ni kumuumiza mwananchi wa kipato cha chini kwenye umasikini.


“Tutaendelea kula mboga za majani hakuna namna kama maisha ndio kila siku yanapanda inabidi tukubaliane na hali lakini ipo haja ya wizara husika kuangalia namna ya kuliweka hili suala sawa, haiwezekani kila siku kukicha nyama inakuwa na bei yake,” amesema Annastela


Nao wauzaji wa nyama waliozungumza na Mwananchi wamesema kupanda kwa nyama hiyo ya ng’ombe ni kutokana na bei wanayouziwa kwenye minada yao, huku wakieleza sababu kuwa ni ng’ombe wengi kuuzwa nchi jirani ya Kenya.


Boniface Roman anayeuza nyama katika soko la Kati, Manispaa ya Moshi amesema ipo haja ya serikali kuangalia namna ya kudhibiti ongezeko kubwa la mifugo kuuzwa nchi za jirani, hali ambayo amesema inasababisha uwepo wa upungufu nyama.


“Ombi letu kwa serikali ni kwamba waangalie na wafuatilie huu mfumuko wa bei kwani inaonekana kuna idadi kubwa ya ng’ombe wanaopelekwa kuuzwa nchi za jirani na kusababisha upungufu wa nyama,” amesema Roman.

Comments